
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito kwa Russia na Ukraine kusimamisha vita katika mstari wa mapigano zilipo hivi sasa, pendekezo ambalo litaiwezesha Moscow kuhodhi sehemu kubwa ya maeneo ya ardhi ya Ukraine.
Trump ametoa wito huo mbele ya waandishi na kueleza kwamba, pande hizo mbili zinapaswa ziache kupigana papo hapo zilipo na kutatua “masuala ya kina”yanayohusu maeneo ya ardhi katika mazungumzo yatakayofanyika hapo baadaye. Mstari wa sasa wa kwenye medani ya vita unapita kwenye eneo la Donbas, kitovu cha viwanda cha Ukraine.
“Ninachosema ni kwamba wanapaswa wasimame hivi sasa hivi kwenye safu za vita, waende zao nyumbani, waache kuua watu na kila kitu kiwe kimekwisha,” amesisitiza rais wa Marekani na kuongeza kuwa itakuwa vigumu kujadiliana kuhusu makubaliano ya mwisho.
Alipoulizwa juu ya nini kitatokea kwa eneo la Donbas, ambalo limeshuhudia mapigano mengi, Trump alisema: “acha likatwe kama lilivyo. limekatwa hivi sasa, nadhani asilimia 78 ya ardhi tayari imechukuliwa na Russia. Unaliacha kama lilivyo hivi sasa. Wanaweza kuja kujadili baadaye kama ilivyo kawaida”.
Ukraine ilikuwa imesisitiza hapo kabla juu ya kurejesha ardhi yake yote.
Aidha itakumbukwa kuwa, Trump mwenyewe alidai mwezi uliopita kwamba Ukraine inaweza kushinda kijeshi na kuteka tena maeneo yote yanayokaliwa na Russia, ambayo yanajumuisha pia Rasi ya Crimea na maeneo mengine ya mashariki mwa Ukraine.
Rais wa Marekani, ambaye aliahidi kuvimaliza haraka vita kati ya Russia na Ukraine, anatazamiwa kukutana na mwenzake wa Russia Vladimir Putin, nchini Hungary mnamo wiki zijazo.
Wiki iliyopita, Trump alimkaribisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy katika Ikulu ya White House na kueleza kwamba, kuna nafasi ya kuhitimisha mzozo huo haraka “ikiwa utaonyeshwa ulegezaji msimamo”…/