
Kuna ‘thank you’ nne zimetembea pale Yanga kwa makocha wake ndani ya kipindi cha takribani siku 337 tangu No-vemba 15, 2024 alipoondoka Miguel Gamondi hadi Oktoba 18, 2025 kwa Romain Folz, lakini bado timu hiyo haijatetere-ka. Imeendelea kuweka utawala wake michuano ya ndani ikizipiga bao Simba na Azam, ambazo ni washindani wake wakubwa.
Katika taarifa kwa umma nne ambazo Yanga imezitoa kwa makocha wake ndani ya kipindi hicho ambao ni Miguel Gamondi, Sead Ramovic, Miloud Hamdi na Romain Folz, bado timu hiyo imekusanya makombe yote ya ndani ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Muungano.
Kidogo kimataifa haijafanya maajabu baada ya msimu uliopita kuishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku msimu huu ikipoteza mechi ya kwanza ugenini kwenye mtoano kuwania kufuzu makundi pia ya michuano hiyo.
Bado marudiano nyumbani.
Yanga inayosaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa tatu mfululizo, juzi Ju-mamosi ilitangaza kuachana na Folz, ikiwa ni saa chache tangu kikosi hicho kitoke kufungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Silver Strikers.
Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilichezwa Uwanja wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Ma-lawi ambapo wenyeji walifunga bao hilo kupitia Andrew Joseph dakika ya 76.
Bado Yanga ina nafasi ya kujitetea katika mechi ya marudiano itakayochezwa Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Ben-jamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao kuanzia 2-0.
Taarifa ya uongozi wa Yanga iliyotolewa Oktoba 18, 2025 imesema:
“Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutaarifu umma kuwa, umevunja mkataba wa Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Romain Folz. Uongozi wa Young Africans SC unamshukuru kocha Romain Folz kwa mchango wake ndani ya klabu yetu na unamtakia kila la kheri katika majukumu yake yanayofata.
“Katika kipindi hiki kikosi chetu kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Patrick Mabedi huku mchakato wa kutafuta Kocha Mkuu ukiendelea.”
Kuondoka kwa Folz, kunaifanya Yanga kufanya mchakato wa kumsaka kocha mkuu huku tayari kukiwa na taarifa za kumalizana na Romuald Rakotondrabe ‘Roro’, aliyekuwa akiinoa timu ya taifa ya Madagascar, ikielezwa amepewa mkataba wa miaka miwili.
Kinachoibeba
Licha ya mabadiliko hayo ya makocha, lakini Yanga imeendelea kufanya vizuri kutokana na kikosi ilichonacho. Hilo lime-jidhihirisha kutokana na aina ya matokeo inayopata tangu wakati Gamondi amechukua mikoba ya Nabi hadi kuon-dolewa kwa Folz licha ya kwamba asilimia kubwa ya makocha waliopita kutokukubalika mbele ya mashabiki wa timu hiyo.
Kikosi kilichoipa Yanga mataji mawili msimu wa 2024-2025, kimefanyiwa maboresho machache ambapo asilimia kubwa wamebaki kuendelea msimu huu.
Djigui Diarra, Khomeiny Abubakar na Aboutwalib Mshery wameendelea kuwa makipa wa kikosi hicho.
Diarra na Mshery, wapo Yanga zaidi ya misimu mitatu, tayari wameweka mizizi klabuni hapo.
Mabeki ni Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Israel Mwenda, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job. Ameondoka Nickson Kibabage huku Yao Attohoula akiwekwa kando akiuguza majeraha.
Eneo hilo, wameongezwa Frank Assinki, Mohamed Hussein na Aboubakar Nizar. Ukiangalia eneo hili nalo, Kibwana, Mwamnyeto, Bacca na Job, nao wamekaa kwa zaidi ya misimu mitatu, kumbuka Job na Bacca ndiyo vitasa vya kuamini-ka kikosini hapo.
Eneo la kiungo wachezaji waliokuwa na timu msimu uliopita hadi sasa ni Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Duke Abuya, Shekhan Khamis na Aziz Andabwile. Pacome na Mudathir, ni zaidi ya misimu mitatu wapo Yanga pia wakicheza kikosi cha kwanza.
Wameondoka Khalid Aucho, Stephane Aziz Ki na Clatous Chama. Wamekuja Abdulnasir Abdallah Mohamed, Moussa Balla Conte, Lassine Kouma na Mohamed Doumbia.
Kwa mawinga, Maxi Nzengeli, Faridi Mussa na Denis Nkane wameendelea kuwepo baada ya kuondoka Jonathan Ikan-galombo, huku Edmund John, Offen Chikola na Celestine Ecua wakitua.
Farid na Nkane sio wachezaji wa kutumika zaidi kikosini, lakini Maxi ambaye huu ni msimu wake wa tatu, ni panga pangua.
Eneo la ushambuliaji, Kennedy Musonda na Jean Baleke wameondoka, wamebaki Clement Mzize na Prince Dube, ki-sha ameongezwa Andy Boyeli.
Dube anakwenda msimu wa pili, lakini Mzize tangu apandishwe timu ya wakubwa, amekuwa mchezaji muhimu huu ukiwa ni msimu wa nne.
Mabadiliko hayo ya wachezaji wachache yanayofanyika kila msimu kwenye maeneo tofauti na kuleta wenye ubora, yanatajwa kuwa ndiyo chachu ya Yanga kutotetereka kama ilivyo kwa wapinzani wake, huku kubwa zaidi ni kukaa na wachezaji bora kwa zaidi ya misimu mitatu.
Siku 337 za mabadiliko
Katika kipindi cha siku 337, Yanga imefanya mabadiliko ya makocha wakuu wanne kwa sababu mbalimbali. Wapo walioondoka kwa makubaliano ya pande mbili kufuatia matokeo mabaya, lakini pia kuna aliyepata dili sehemu nyingine na mkataba kumalizika.
Baada ya Yanga kuwa kwenye mafanikio makubwa chini ya Nasreddine Nabi, kocha Mtunisia aliyeipeleka timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022–2023 ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo, akaondoka mwisho wa msimu huo, kijiti akakabidhiwa Miguel Gamondi raia wa Argentina.
Gamondi aliyetokea Ittihad Tanger ya Morocco, hakuanza vizuri msimu wa 2023-2024 kwani alipoteza Ngao ya Jamii mbele ya Simba, lakini mwisho wa msimu akabeba Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Kocha huyo ambaye baada ya kuondoka Yanga Novemba 15, 2024, amepata dili la kuinoa Singida Black Stars alipo sasa tangu mwanzoni mwa msimu huu.
Ndani ya Yanga, Gamondi aliiongoza timu hiyo kucheza mechi 40 za Ligi Kuu Bara, akishinda 34, sare 4 na kupoteza 4.
Yanga ilifunga mabao 85, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18. Alikusanya jumla ya pointi 104 katika mechi hizo 40.
Gamondi ameondoka Yanga akishinda mataji matatu, akianza na Ligi Kuu Bara na Kombe la FA yote msimu wa 2023-2024, kisha Ngao ya Jamii kufungua msimu wa 2024-2025 ambao uliishia njiani baada ya kuondoka Novemba 2024.
Pia aliipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita takribani miaka 25. Kwa kuonye-sha hakubahatisha, akarudia kufanya hivyo msimu uliofuatia 2024-2025, ingawa hakuiongoza hata mechi moja ya ma-kundi. Akawa ameondolewa.
Sead Ramovic
Alitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini, kwa sasa yupo CR Belouizdad ya Algeria baada ya kuondoka Yanga Februari 4, 2025.
Kocha huyo alitua Yanga Novemba 15, 2024 kuchukua mikoba ya Gamondi. Akakiongoza kikosi kwenye jumla ya mechi 13 za mashindano yote ikiwemo sita ya Ligi Kuu Bara aliyoshinda yote, sita Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi akishinda mbili, sare mbili na kupoteza mbili, pia mechi moja ya Kombe la FA akishinda pia.
Jumla, alisimamia mechi 13, akishinda tisa, sare mbili na kupoteza mbili, timu ilifunga mabao 32 na kuruhusu manane. alikaa Yanga kwa siku 81, ikiwa ni takribani miezi miwili na siku 19 pekee, hakushinda taji lolote.
Miloud Hamdi
Alitokea Singida Black Stars iliyomtambulisha Desemba 30, 2024. Kabla ya kutua nchini kujinga na Singida Black Stars, mara ya mwisho alikuwa Al-Khaldiya FC ya Bahrain, kwa sasa anainoa Ismaily SC ya Misri baada ya kuachana na Yanga mkataba wake ulipomalizika mwishini mwa msimu wa 2024-2025.
Hamdi aliyetua Yanga Februari 4, 2025, ameondoka kikosini hapo akiwa ameiongoza katika mechi 13 za Ligi Kuu Bara akishinda 12 na kutoka sare moja, huku akivuna jumla ya mabao 41 na kufungwa matatu tu.
Akabeba kombe.
Kocha huyo aliiongoza Yanga katika mechi tano za Kombe la FA kuanzia hatua ya 32 Bora hadi fainali akishinda zote akivuna mabao 17 na kufungwa moja tu na kutetea taji hilo.
Katika Kombe la Muungano, kocha huyo aliiongoza Yanga kucheza mechi tatu akishinda zote, akianza kwa kuifunga KVZ kwa mabao 2-0, kisha kuing’oa Zimamoto kwa penalti 3-1 baada ya sare ya 1-1 ya dakika 90 na katika fainali ikaichapa JKU kwa bao 1-0 na kutwaa ubingwa.
Hilo lilikuwa kombe la kwanza kushinda ndani ya kikosi cha Yanga, kisha ikafuata Ligi Kuu Bara.
Hii ikiwa na maana katika siku 148 alizoiongoza Yanga kama kocha mkuu, Hamdi amecheza jumla ya mechi 21 za mashindano yote, timu hiyo ikishinda 19 na kutoka sare mbili ikiwamo ile na nusu fainali ya Kombe la Muungano kabla ya kuvuka kwa penalti kwenda fainali na ile ya JKT Tanzania.
Hamdi aliyekaa kwa takribani siku 153, ikiwa ni miezi mitano na siku tatu, alihitimisha na Kombe la FA alipoichapa Sin-gida Black Stars mabao 2-0 kwenye mechi ya fainali.
Romain Folz
Ametokea Olympique Akbou ya Algeria akiwa Mkurugenzi wa Ufundi. Kibarua chake kimesitishwa Oktoba 18, 2025, ikiwa ni takribani siku 96 amehudumu klabuni hapo ikiwa ni miezi mitatu na siku nne.
Folz hajaondoka kinyonge, ametwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0. Jumla ameiongoza timu hiyo katika mechi sita za mashindano, akishinda nne, sare moja na kupoteza moja. Timu hiyo imefunga mabao tisa na kuruhusu moja pekee.