Dar es Salaam. Kwa takribani miaka 15 katika muziki wa Bongo Fleva, Darassa, ambaye anasimamiwa na menejimenti yake ya Classic Music Group (CMG), ameendelea kuwaburudisha na kuwaelimisha mashabiki wake, kama ulivyo msingi wa jina lake.

Darassa ni mmoja wa wasanii wa Rap wanaouza zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania. Namba zake za mauzo zipo juu kuliko wasanii wengi wa Rap, ameweza kutoa albamu, kushinda tuzo, na kuendelea kudhihirisha umahiri wake katika sanaa ya muziki. Fahamu zaidi.

1. Ben Pol ndiye msanii aliyechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Darassa. Kwanza, kwenye wimbo uliomtoa Darassa ‘Sikati Tamaa’, Ben Pol ndiye aliyeimba kiitikio. Pili, kwenye wimbo mkubwa zaidi wa Darassa, ‘Muziki’, Ben Pol pia ndiye aliyehusika kwenye kiitikio.

2. Hadi sasa, video ya wimbo wa Darassa, Muziki (2016), inashikilia rekodi ya kuwa video ya msanii wa rap au hip hop Bongo iliyotazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube.

Ngoma hiyo iliyotayarishwa na Mr Vs, Abbah na Mr T Touch, video yake imetazamwa mara milioni 31 ikiwa imeipita ile ya AY akiwa na Diamond Platnumz, Zigo Remix (2016).

3. Kolabo yake na Bien, mwanachama wa kundi la Sauti Sol kutoka Kenya, No Body (2023) imesikilizwa zaidi ya mara milioni 18.1 huko Boomplay na ndio wimbo wa kwanza na wa pekee kwa Darassa kufikia mafanikio hayo.

4. Darassa ana tabia ya kipekee katika uandishi wa nyimbo zake. Huwezi kumkuta anaandika wimbo bila kusikia mdundo kwanza. Tofauti na wasanii wengi wanaoandika kwanza kisha kutafuta biti yeye hufanya kinyume chake.

5. Mwaka 2020, albamu ya Darassa ‘Slave Becomes a King’ ndio ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya nyimbo nyimbo 21. Albamu hiyo ilifuatiwa na Afro East ya Harmonize yenye nyimbo 18, na Story of The African Mob ya Navy Kenzo yenye nyimbo 12.

6. Wakati Darassa anatoa wimbo wake, Sikati Tamaa (2012), alikuwa akiwasiliana na Director Hanscana kupitia Facebook kama shabiki tu. Baadaye, Hanscana ndiye aliyekuja kutengeneza video nyingi za Darassa kama Too Much, Kama Utanipenda, Hasara Roho, Muziki, Leo, Relax, Tumepoteza na kadhalika.

7.  Tuzo ya kwanza na ya pekee kwa Darassa kushinda katika TMA ni kupitia wimbo wake ‘Loyalty’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Slave Becomes a King (2020) akiwa na Nandy na Marioo ulioshinda kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2021.

8. Jina ‘Darassa alipewa na Hayati Complex pamoja na wasanii aliowakuta studio, ni baada ya kutoa maoni yenye uzito na kuelimisha katika mjadala. Wote walikubaliana majibu yake yalikuwa kama ya mwalimu, ndipo wakamuita Darasa.

9. Alikiba kutokaa Kings Music ndiye mwanamuziki pekee ambaye amesikika katika albamu zote mbili za Darassa, Slave Becomes a King (2020) na Take Away The Pain (2025).

10. Darassa ndiye msanii anayefanya vizuri Boomplay akiwa amesikilizwa zaidi ya mara milioni 83.4, huku akifuatiwa na Billnass, rapa aliyetoka na ngoma, Raha (2016) akiwa na TID na Naziz, mwanachama wa kundi la Necessary Noize kutokea Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *