Mapema Jumatatu msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amewaambia waandishi wa habari kwamba Waziri Mkuu Netanyahu amekutana na mjumbe maalum Steve Witkoff na mkwe wa Rais Donald Trump, Jared Kushner.
Ziara hiyo nchini Israel inalenga kufanya ukaguzi juu ya maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa usitishaji wa mapigano uliopatikana siku chache zilizopita.
Wajumbe hao wanaizuru Israel saa chache baada ya Israel kutangaza kukifungua tena kituo cha upitishwaji wa misaada ya kibinadamu cha Kerem Shalom baada kufungwa siku ya jumapili kwa madai kwamba Hamas walikiuka makubaliano ya usitishwaji wa vita yaliyosainiwa kwa kuwashambulia wanajeshi wa Israel waliokuwa kusini mwa Gaza na kufanya mauaji ya askari wawili.
Na kama njia ya kulipiza kisasi Israel ilifanya mashambulizi huko Gaza ambayo kwa mujibu wa hospitali za Gaza yaliwaua wapalestina 45.
Pande zote mbili hata hivyo zimesisitiza kwamba bado zinaendelea kutelekeza maazimio yaliyofikiwa kwenye makubaliano ya usitishwaji wa vita.
Ben Gvir: Lazima tuisambaratishe Hamas
Kwa upande mwingine, Waziri wa masuala ya usalama waIsrael, Itamar Ben Gvir ameendelea kusisitiza kwamba malengo ya Israel ni kuisambaratisha kabisa Hamas.
“Hili ndilo lengo la vita, hili ndilo jambo la muhimu zaidi – kuivunja Hamas, bila kujali ni kwa gharam gani. Ni Kuivunja, ili isiwepo. Waziri Mkuu aliniahidi, na nitasisitiza juu yake katika kikao hiki cha bunge kwamba hiki ndicho atakachofanya. Natoa wito kwa waziri mkuu, ni wakati wa kurejea vitani, kuvunja vunja, na kusambaratisha kila kitu ili kushinda.” amesema Ben Gvir.
Jumatatu ya leo pia ujumbe wa Hamas unatarajiwa kukutana na maafisa wa Qatar na Misri mjini Cairo ili kujadili namna ya kuendelea kutelekeza maazimio ya usitishaji vita wa Gaza, hayo yamesemwa na chanzo kilicho karibu na mazungumzo hayo kwa shirika la habari la AFP.
Makamu wa rais wa Marekani JD Vance nae anatarajiwa pia kuitembelea Israel hivi karibuni.