OFISA Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kimeweka dhamira kubwa kuelekea mechi ya marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, akisisitiza kuwa hii ni mechi ya kihistoria kwa klabu hiyo na haipaswi kuchukuliwa kwa urahisi.

Simba inatarajia kushuka dimbani Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3–0 ilioupata kwenye mechi ya kwanza ugenini. Hata hivyo, Ally amewaonya mashabiki kutoiona kama mechi rahisi.

“Kwetu huu ni mchezo muhimu kwelikweli. Ni mchezo unaoenda kuandika historia ya kupendeza. Tunaenda kujiweka katika kundi la vilabu (klabu) vikubwa barani Afrika vyenye uhakika wa kucheza hatua ya makundi kila mwaka,” amesema Ally.

Amefafanua kuwa, Simba ipo katika njia ya kujiunga na klabu mbili pekee zilizoonyesha ubora katika michuano ya CAF ndani ya miaka saba iliyopita, akizitaja kuwa ni Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

AHM 01

“Katika kipindi cha miaka saba, timu ambazo zimekuwa na uhakika wa kucheza makundi ni Al Ahly na Mamelodi. Lakini sasa wa tatu anaenda kuongezeka na huyo ni Simba. Hiyo ni heshima kubwa sana kwetu.”

Ally amesema mechi hiyo sio ya kawaida kwa sababu inawakilisha hadhi na heshima ya klabu ndani ya bara la Afrika, hivyo kila shabiki anatakiwa kulitambua hilo.

“Mwanasimba hatakiwi kwa namna yoyote kubaki nyumbani. Hatutaki mtu aseme ‘tumeshinda ugenini, tumemaliza kazi.’ Hapana! Hii mechi ni kama hatujacheza bado,” amesema.

Katika mkutano huo na wanahabari, Simba imetangaza viingilio ambapo Jukwaa la Mzunguko ni Sh5,000, VIP C Sh10,000, VIP B Sh20,000, VIP A Sh30,000, Platinum Sh150, 000 na Tanzanite Sh250,000.

AHM 02

Rekodi zinaonyesha katika miaka saba ambayo Ahmed Ally ameizungumzia, Simba imecheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF mara tano ambayo ni msimu wa 2020–2021 (Ligi ya Mabingwa), 2021–2022 (Kombe la Shirikisho), 2022–2023 (Ligi ya Mabingwa), 2023–24 (Ligi ya Mabingwa) na 2024-2025 (Kombe la Shirikisho). Ikifuzu safari hii itakuwa ya sita mfululizo inakwenda kucheza makundi.

Katika mara zote hizo ilizofuzu makundi, pia imefanikiwa kwenda hadi robo fainali na kuishia hapo, lakini msimu uliopita 2024-2025 ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipoteza mbele ya RS Berkane. Kabla ya hapo, Simba pia ilicheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018–2019.

Kwa upande wa Mamelodi Sundowns, rekodi zinaonyesha timu hiyo kutoka Afrika Kusini, tangu mwaka 2016 imekuwa na uhakika wa kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Rekodi hizo zinaonyesha mwaka 2016 ilitwaa ubingwa, kisha 2017 (robo fainali), 2018 (makundi), 2018–19 (nusu fainali), 2019–20 (robo fainali), 2020–21    (robo fainali), 2021–22    (robo fainali), 2022–23 (nusu fainali) na 2023–24 (nusu fainali).
Kwa Al Ahly, klabu yenye historia nzuri na Ligi ya Mabingwa Afrika ikibeba taji hilo mara 12, imekuwa ikifanya vizuri mfululizo katika michuano hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *