
Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amesema, vita vya utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza si kitu kingine ila ni mauaji ya kimbari sambamba na kuulaani utawala huo ghasibu kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Akihutubia katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Shura, ambalo ni baraza la kutunga sheria la Qatar, Sheikh Tamim amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa lazima iwape ulinzi watu wa Palestina na kuhakikisha kuwa wahusika wa mauaji ya kimbari hawakwepi uwajibikaji.
“Inasikitisha kwamba jamii ya kimataifa inabaki kuwa haina uwezo wa kutekeleza hatua za kupatikana heshima linapokuja suala la maafa ya watu wa Palestina,” ameeleza Amir huyo wa Qtar.
Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amebainisha kwa kusema: “tunatilia mkazo msimamo wetu wa kulaani ukiukaji na vitendo vyote vya Israel huko Palestina, hususan kuugeuza Ukanda wa Ghaza kuwa eneo lisiloweza kukaliwa na watu, kuendelea kukiuka usitishaji vita, kupanua vitongoji katika Ukingo wa Magharibi, na kujaribu kuliyahudisha eneo la Msikiti mtukufu wa Al-Aqsa.”
Kadhalika, Amir wa Qatar amesema: “tunathibitisha pia kwamba Ukanda wa Ghaza ni sehemu isiyotenganika ya maeneo ya Palestina ya nchi moja iliyoungana ya Palestina”…/