
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres wamefanya mazungumzo ya simu na kuzungumzia matukio ya kikanda ikiwemo hali ya Gaza na Yemen.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Waziri Araghchi amesisitiza juu ya wajibu wa jamii ya kimataifa wa kuizuia Israel kuendelea kukiuka usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, na kuwezesha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa eneo lililozingirwa.
Akizungumzia hali ya Yemen, Sayyid Araghchi amelaani hujuma za Israel dhidi ya nchi hiyo na kusisitiza dhamira ya Iran ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa kusaidia kuweka utulivu nchini Yemen, na kulinda usalama wa eneo hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa upande wake, ameshukuru na kupongeza juhudi za kidiplomasia za Iran katika kuunga mkono amani na utulivu wa kikanda, na kutoa wito wa kuendelezwa kwa mashauriano yenye lengo la kurejesha utulivu na usalama nchini Yemen na eneo zima la Asia Magharibi.
Guterres, mbali na kupongeza ushirikiano wa kidiplomasia wa Iran, ametoa wito wa mazungumzo na ushirikiano endelevu ili kudumisha amani na utulivu nchini Yemen na Mashariki ya Kati.
Mazungumzo hayo ya simu yamefanyika katika hali ambayo, Israel imewaua shahidi Wapalestina 97 na kujeruhi 230 tangu makubaliano ya usitishaji wa mapigano yaanze kutekelezwa Oktoba 10, kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza.
Israel pia imekuwa ikifanya mashambulizi ya kuogofya ya anga katika maeneo yote ya Yemen, kinyume cha sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.