London, England. Kabla hujacheza na kikosi cha Diego Simeone, jambo la kwanza unalotakiwa kujua ni kwamba hutakiwi kuwakasirisha. Lakini Arsenal imefanya hivyo, na sasa Atletico Madrid imepeleka malalamiko rasmi kwenye Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) baada ya kukosa maji ya moto kwenye vyumba vyao vya kubadilishia nguo uwanjani Emirates.

Tukio hilo limetokea jana Jumatatu jioni wakati Atletico ilipokuwa ikifanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal. Baada ya mazoezi, wachezaji walitaka kuoga lakini wakagundua maji yote ni baridi.

Mvua ilikuwa imenyesha, hivyo wachezaji walilazimika kupanda kwenye basi lao na kurudi hotelini kuoga huko. Awali waliijulisha Arsenal kuhusu tatizo hilo, lakini klabu hiyo ya London haikuweza kulitatua kwa wakati kwani maji ya moto yalirejea muda mfupi baada ya Atletico kuondoka.

Hali hiyo imewakera viongozi na wachezaji wa Atletico, ambao wanasema ni aibu kwa klabu kubwa kama Arsenal kushindwa kuweka mazingira mazuri kwa wageni. Hivyo wakaamua kuandika barua rasmi kwenda UEFA.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za UEFA, timu mwenyeji inapaswa kuhakikisha kuna maji ya moto kwenye vyumba vya kubadilishia nguo siku ya mechi, lakini kanuni hizo hazihusiani na siku za mazoezi. Hivyo, Arsenal huenda isiadhibiwe kutokana na malalamiko ya Atletico.

Arsenal tayari imeomba radhi kwa Atletico kwa usumbufu huo, wakidai ilikuwa hitilafu ya ghafla kwenye mfumo wa maji ya moto.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, licha ya sintofahamu hiyo, amezungumza kwa maneno ya heshima kuhusu Simeone kabla ya mechi:

“Ni kocha ninayemheshimu sana. Amekaa kwenye klabu moja muda mrefu, bado ana hamasa na anawajenga wachezaji wake kila siku. Ni jambo la kipekee sana,” amesema Arteta.

Arteta pia amesema anavutiwa na nidhamu na namna Atletico wanavyopambana uwanjani:

“Wanacheza kwa nidhamu ya hali ya juu, kila mchezaji anapambana kwa kila mpira. Ukiangalia wanavyoshindana, unajua ni timu inayojua wanachotaka.”

Arsenal itavaana na Atletico leo saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Emirates, London katika michuano hiyo mikubwa Ulaya.

Mara ya mwisho Arsenal kukutana na Attletico ilikuwa msimu wa 2017-2018 kwenye mashindano ya Europa League ambapo Arsenal iliondolewa katika hatua ya nusu fainali baada ya kutupwa nje kwa jumla ya mabao 2-1.

Mechi ya kwanza Arsenal ililazimishwa sare ya 1-1 jijini London kabla ya kukubali kipigo cha bao 1-0 ilipoenda ugenini kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano, Madrid, Hispania.

Hata hivyo, kocha Arteta amekuwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za Hispania kwani tangu ajiunge na Washika mitutu hao wa London, ameiongoza Arsenal kushinda mechi sita za mwisho ilipokutana na timu tofauti za Hispania.

Arsenal imeifunga Real Madrid mara mbili, Sevilla mara mbili, Girona na Athletic Club mara moja.

Mechi nyingine za Ligi ya Mabingwa Ulaya

Barcelona vs Olympiacos

Kairat Almaty vs Pafos

Arsenal FC vs Atlético Madrid

Bayer Leverkusen vs Paris Saint-Germain

Copenhagen vs Borussia Dortmund

Newcastle United vs Benfica

PSV Eindhoven vs Napoli

Union Saint-Gilloise vs Inter Milan

Villarreal CF vs Manchester City

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *