BAADA ya Dar City kufuzu kucheza hatua ya pili ya mashindano ya Road to BAL Divisheni ya Mashariki, kocha wa timu hiyo Mohamed Mbwana amezungumzia mambo kadhaa, lakini akitaja kile wanachokwenda kukifanya ili kuipeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano hayo makubwa Afrika.
Mbwana ameliambia Mwanaspoti kuwa sababu iliyofanya timu yake ifuzu ni kutokana na viwango vikubwa vya wachezaji waliona kikosini ambao wana uwezo mkubwa wa kusoma mchezo na kuamua namna gani ya kukabiliana na wapinzani wao na kwamba hicho ndicho wanakwenda kukitumia katika hatua inayofuata.
Amesema kwamba mbinu mpya za kiufundi wanazotarajia kuja nazo zinakusudiwa kukifanya kikosi hicho kufanya vizuri zaidi.
Akitoa mfano katika mchezo dhidi ya Namuwongo Blazers ya Uganda ambao na mwanzoni ulianza kuonyesha upinzani mkali, wachezaji wake walibadilika na kuanza kutumia nafasi chache walizozipata kuhakikisha kwamba wanapata matokeo mazuri.
Amesema walianza kuongozwa katika robo ya kwanza kwa pointi 32-22, huku akiamini ingeweza kuwa mechi ngumu kushinda, lakini benchi la ufundi lilipomwingiza Amin Mkosa alienda kusaidia kubadili matokeo na hatimaye ushindi ulipatikana.
“Tulivyoona kuna sehemu yenye kasoro tulimwingiza Amin Mkosa aliyeweza kudhibiti eneo la ulinzi na kufanya timu ya Dar City ishinde kwa pointi 83-70,” amesema Mbwana akiwataja baadhi ya wachezaji wa kigeni waliowasajili kwa ajili ya mashindano hayo na walioonyesha viwango vikubwa kuwa ni pamoja na Solo Diabate ambaye ni raia wa Ivory Coast alitewahi pia kuichezea timu ya kikapu ya Zamalek ya Misri na US Monastri ya Tunisia. Mchezaji huyo anayecheza namba moja maarufu kama ‘point guard’ alikuwa kivutio kutokana na jinsi alivyomiliki eneo la kati na kutoa asisti kwa wafungaji.
Mbali ya kutoa asisti pia alionyesha uwezo mkubwa wa kudunda mpira na kupenya mbele ya walinzi wa timu pinzani bila kuzuiwa kirahisi. Wengine ni Deng Angoko raia wa Sudan Kusini, Makh Mitchell na Raphaiel Putney (Marekani) walioshirikiana na Mkosa, Hasheem Thabeet na Ally Abdalah kuhakikisha kwamba ushindi unapatikana, na kwamba hiyo ndiyo silaha yao katika mechi zijazo.

Naye kamishna wa makocha wa Shirikisho la Kikapu Tanzania, Robert Manyerere amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Dar City ulichangia kufuzu hatua hiyo kwenye mashindano hayo.
Manyerere amesema licha ya Namuwongo Blazers kuwa na uwekezaji mkubwa, lakini mastaa wake walikwama mbele ya Dar City kutokana na kushindwa kusoma vyema mchezo. Timu hiyo ina wachezaji wakali akiwamo Raphaiel Putney ambaye ni raia wa Marekani aliyefunga pointi 55 peke yake katika mchezo dhidi ya Djabar ya Comoro.
Aliwataka wachezaji wazawa ambao hawajapata nafasi ya kucheza kwenye mashindano hayo kujifunza kupitia wageni na wazawa walionao kikosini ambao wamekuwa bora kusoma mechi na kuamua namna ya kusaka matokeo ya ushindi.
“Inawapaswa kujifunza huku mkiwa na malengo ya kucheza. Haya ni mashindano ya kimataifa na yenye ushindani,” amesema Mayerere. Dar City ilifuzu hatua inayofuata baada ya kuishinda Djabar kwa pointi 102-50 na Namuwongo Blazers 83-70.
Kwa matokeo hayo Dar City na Namuwongo Blazers zimefuzu kucheza hatua ya pili. Mashindano hayo yanapigwa katika Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Masaki jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Dar City, Simon Joe amesema tarehe mpya ya mashindano hayo itatangazwa hivi karibuni na mara hii yakiitwa Elite 16, ambapo yatakutanisha timu mbili zilizofuzu katika kundi kila kundi yaani A, B, C, D na E zitakazoungana na zingine sita zilizopita, huku mbili zitakazofanya vizuri zitashiriki mashindano ya BAL 2026.
MWANASPOTI YAPEWA TUZO BDL
CHAMA cha Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), kimetambua mchango wa gazeti la Mwanaspoti katika kuitangaza Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ambapo limelitunuku tuzo ya mwaka 2025.
BD imetoa tuzo ya cheti kwa Mwanaspoti, ambapo akizungumzia sababu zilizokifanya chama hicho kufanya hivyo, katibu mkuu Mpoki Mwakipake amesema inatokana na kazi nzuri iliyofanywa na gazeti hilo katika kutoa taarifa za BDL wakati mechi zikichezwa.
“Kwa kweli tunashukuru sana kwa mchango mkubwa uliotolewa na gazeti hili. Imetugusa na hivyo tunatoa cheti kwa gazeti la Mwanaspoti,” amesema Mpoki.

Naye kamishna wa makocha wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), Robert Manyerere amesema BD inatambua kazi kubwa inayofanywa na gazeti hili katika kuutangaza mpira wa kikapu.
Manyerere amesema Mwanaspoti limekuwa likitangaza pia ligi za kikapu zinazofanyika mikoani na kwamba, hii ni mara ya pili kwa gazeti hili kupewa cheti cha kutambuliwa mchango wake kwani ile ya kwanza ilikuwa ni 2023.
Akizungumzia tuzo hiyo, mwandishi wa Mwanaspoti, Brown Msyani amesema gazeti hili limekuwa likiitangaza michezo yote nchini ambayo vyombo vingine vya habari haviifikii wala kuitangaza.

MAANDALIZI YAIATHIRI BANDARI TANGA
NYOTA wa timu ya Bandari Tanga, Riziki Mgude ametoa sababu iliyofanya ishindwe kutinga fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Tanga kwamba ni kutokana na kutokuwa maandalizi mazuri.
Mgude ambaye pia ni kocha wa Bandari Queens, amesema nguvu zao kwa sasa wanazielekeza katika mashindano ya Bandari na Shimmuta.
“Unajua kama tungekuwa na maandalizi ya kutosha naamini tungetinga fainali bila kikwazo,” amesema Mgude
Timu ya Bandari Tanga ilifungwa na Ngamiani Kings mara mbili kwa pointi 75-68, 53-49 na Deep Sea 58-51 na 64-47. Akizungumzia kuhusiana na Bandari Queens iliyoingia fainali, amesema inatokana na uzoefu mkubwa wa wachezaji ilionao tofauti na timu zingine zilizoshiriki ligi hiyo.