Uwanja huo wa ndege ulikuwa umefungwa tangu kulipozuka mapigano Aprili 2023, kati ya Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye miundombinu muhimu na hasa kwenye mji mkuu Khartoum.
Mashuhuda wameliambia shirika la habari la AFP kwamba walisikia milio ya droni kwenye eneo la katikati na kusini mwa Khartoum pamoja na milipuko ya makombora kwenye eneo la uwanja wa ndege majira ya saa 10 hadi saa 12 asubuhi, kwa saa za maeneo hayo.
Mmoja ya mashuhuda hao anayeishi kwenye viunga vya Al-Azhari kusini mwa Khartoum amesema alisikia mlipuko na kisha droni ikapita juu kwenye eneo hilo. Mkaazi mwingine wa eneo la katikati mwa Khartoum amesema aliamshwa na milio ya droni majira ya saa 10 za alfajiri. Muda mfupi baadae alisikia vishindo vikubwa kwenye eneo la uwanja wa ndege.
Siku ya Jumatatu, Mamlaka ya Anga ya Sudan ilisema uwanja huo wa ndege utafunguliwa tena siku ya Jumatano, na safari za ndani zitaanza kurejea baada ya maandalizi ya kiufundi na kiuendeshaji kukamilika.
Khartoum imeendelea kuwa tulivu chini ya jeshi
Khartoum imeendelea kuwa na utulivu tangu jeshi liliporejesha udhibiti mapema mwaka huu, ingawa mashambulizi ya droni yameendelea. RSF wamekuwa wakilaumiwa mara kwa mara kwa kuwalenga wanajeshi na miundombinu ya umma.
Shuhuda mwingine ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kwamba droni zilishambulia kwenye maeneo ya kaskazini mwa Omdurman mapema hii leo. Eneo hilo linajulikana kwa kuwa na kambi kubwa zaidi za kijeshi. Hakuna yoyote aliyekiri kufanya mashambulizi hayo na hakuna taarifa zozote za uharibifu, majeruhi ama vifo.
Shambulizi hili la leo Jumanne, ni la tatu kwenye mji huo mkuu katika kipindi cha wiki moja. Wiki iliyopita, droni zilifanya mashambulizi kwenye mji huo wa Khartoum kwa siku tano mfululizo, ikiwa ni pamoja na yale yaliyofanyika kwenye kambi mbili za kijeshi zilizoko magharibi mwa mji. Lakini afisa mmoja wa kijeshi alisema droni nyingi zilidunguliwa.
Karibu watu 800,000 wamerejea kwenye mji wa Khartoum tangu jeshi liliporejesha udhibiti wake. Serikali pia imeanza kuwarudisha maafisa waliohamia kwenye mji wa bandari waPort Sudan ambako walikuwa wakifanya shughuli zao wakati wa mapigano.
Khartoum ni mji uliojaa vifusi kutokana na mapigano
Sehemu kubwa ya Khartoum ni vifusi, na mamilioni ya wakazi bado wanakumbwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara kunakodaiwa kusababishwa na mashambulizi ya droni yanayofanywa na RSF.
Umoja wa Mataifa umeonya siku ya Jumatatu kuhusu kuongezeka kwa machafuko kaskazini na magharibi mwa Darfur, kufuatia mashambulizi haya ya droni na mapigano ya ardhini.
Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya raia na wengine karibu milioni 12 wakiwa wameyakimbia makaazi yao, hatua inayoibua mzozo mkubwa kabisa wa kukosa makaazi na njaa ambao haujashuhudiwa ulimwenguni.