Rais wa Marekani Donald Trump alipowasilisha mpango wake wa kusitisha mapigano Gaza, wengi hawakutarajia kwamba msukumo mkubwa wa makubaliano hayo ungetokea Ankara.

Kwa kuishawishi Hamas kuukubali mpango huo wa Marekani, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameibadilisha nchi yake kutoka kuwa mtazamaji hadi kuwa mdau mkuu wa diplomasia ya Mashariki ya Kati.

Mara moja, uhusiano wa karibu wa Uturuki na Hamas — ambao zamani ulionekana kuwa mzigo wa kisiasa kwa Washington — sasa umegeuka kuwa silaha ya kisiasa inayoongeza ushawishi wake wa kimataifa.

Kutoka mpatanishi hadi mdau mkuu wa nguvu

Awali, viongozi wa Hamas walikataa shinikizo la Marekani la “kuwaachia mateka wa Kiyahudi au kukabiliana na maangamizi zaidi.” Lakini baada ya Ankara kuingilia kati, kundi hilo lilikubali masharti hayo.

Vyanzo viwili vya kanda na maafisa wawili wa Hamas waliiambia Reuters kwamba ujumbe wa Uturuki ulikuwa wazi: ni wakati wa kukubali.

Trump alimsifu Erdogan akisema: “Mtu huyu kutoka sehemu inayoitwa Uturuki ni mmoja wa wenye nguvu zaidi duniani. Ni mshirika wa kuaminika — kila ninapomhitaji yupo.”

Saini ya Erdogan kwenye hati ya makubaliano ya Gaza imeongeza kasi ya juhudi za Uturuki kurejesha nafasi yake kuu katika siasa za Mashariki ya Kati — jambo lililozitia wasiwasi Israel, Misri, Saudi Arabia, na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Misri, Sharm el-Sheikh 2025 | Erdogan na Trump washiriki katika mkutano wa amani kuhusu Gaza
Rais Donald Trump akiteta jambo na Rais Erdogan wakati wa mkutano wa amani kuhusu Gaza, mjini Sharm el-Sheikh, Misri, Oktoba 13, 2025.Picha: Mustafa Kamaci/Tur Presidency/Anadolu Agency/IMAGO

Nguvu mpya na ushawishi mpya Washington

Kwa Erdogan, mafanikio haya ni zaidi ya sifa za kidiplomasia. Ni nafasi ya kujenga upya ushawishi wa Uturuki mbele ya Marekani.

Sinan Ulgen, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti ya EDAM mjini Istanbul, anasema uamuzi wa Ankara kuishawishi Hamas umetoa nafasi mpya ya kisiasa na kiuchumi.

“Kama sifa hizo kutoka kwa Trump zitadumu, Uturuki inaweza kutumia fursa hii kutatua migogoro ya muda mrefu,” Ulgen aliiambia Reuters.

Miongoni mwa mambo ambayo Ankara inataka ni kurudishwa kwenye mpango wa ndege za kivita za F-35, kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani, na msaada zaidi katika masuala ya usalama nchini Syria.

Kumbukumbu za Ufalme wa Ottoman

Uhusiano kati ya Washington na Ankara ulianza kubadilika wakati Erdogan alipotembelea Ikulu ya White House mwezi Septemba — ziara yake ya kwanza baada ya miaka sita.

Mazungumzo yao yalihusu masuala tete kama vikwazo vya Marekani kufuatia ununuzi wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi chapa S-400, na ushirikiano wa Marekani na wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria.

Sasa, Ankara inaonekana kupata matokeo. Kamanda wa vikosi vya SDF, Mazloum Abdi, amethibitisha mpango wa kuviunganisha na jeshi la Syria — hatua ambayo Uturuki inaona kama ushindi wa kimkakati.

Marekani, Washington D.C. 2025 | Mkutano kati ya Donald Trump na Recep Tayyip Erdogan katika Ikulu ya White House
Rais Trump amemtaja Erdogan kama mmoja ya viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani, na kumsifu kuwa mtu ambaye hajawahi kumuangusha.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Makubaliano ya Gaza yameongeza hadhi ya Uturuki katika diplomasia ya kimataifa. Trump amemsifu Erdogan kwa kuandaa mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine, na baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad mwaka 2024, Ankara ilionekana tena kuwa na nguvu kubwa katika kanda.

Kwa wakosoaji wake, hili linaamsha kumbukumbu za Ufalme wa Ottoman, iliyotawala sehemu kubwa ya Mashariki ya Kati karne moja iliyopita. Nchi nyingi za Kiarabu zinahofia huenda Uturuki ikarejea katika siasa za kikanda kwa mtazamo wa utawala wa zamani.

“Erdogan ni bingwa wa kupanua ushawishi wake — akitumia matukio kwa faida yake binafsi,” alisema mchambuzi wa kisiasa wa Kiarabu Ayman Abdel Nour. “Nchi za Ghuba hazikufurahia Uturuki kuongoza mazungumzo ya Gaza, lakini zilihitaji vita vikome.”

Uamuzi wa Trump ulibadilisha mchezo

Vyanzo vya kidiplomasia vinasema Israel mwanzoni ilikataa Uturuki kushiriki katika mazungumzo, lakini Trump aliingilia kati moja kwa moja na kuruhusu Ankara kushiriki.

Mkuu wa ujasusi wa Uturuki Ibrahim Kalin aliongoza mazungumzo ya faragha, akiihakikishia Hamas kuwa mpango huo unaungwa mkono na Marekani, Misri, na Qatar — kwa ahadi binafsi kutoka kwa Trump.

Afisa mmoja wa Hamas alisema: “Dhamana pekee ya kweli ilitoka kwa pande nne: Uturuki, Qatar, Misri, na Wamarekani. Trump aliahidi kibinafsi kwamba hakutakuwa na kurejea vitani.”

Makubaliano hayo yalihakikisha kuachiwa kwa mateka wa Kiyahudi waliotekwa Oktoba 7, 2023, katika shambulio lililoua watu 1,200, huku zaidi ya Wapalestina 67,000 wakiuawa baadaye katika mashambulizi ya Israel, kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza.

Marekani, Washington D.C. 2025 | Mkutano kati ya Donald Trump na Recep Tayyip Erdogan katika Ikulu ya White House
Rais Donald Trump (kulia katikati) akizungumza wakati wa mkutano na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kushoto katikati) katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House, Alhamisi, Septemba 25, 2025, mjini Washington.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Uturuki yarejea kwenye ramani ya nguvu

Je, makubaliano haya yatakuwa njia ya kuelekea amani ya kudumu au suluhisho la mataifa mawili?

Wadhamini kama Uturuki, Misri, na Qatar wanasema mpango huo hauna ramani ya kisiasa kuelekea taifa la Palestina.

Erdogan amesema mazungumzo kuhusu uwezekano wa jeshi la Uturuki kushiriki katika ujenzi wa Gaza yatajadiliwa baadaye. Kipaumbele chake kwa sasa ni “kusitisha mapigano kabisa, kuruhusu misaada, na kuijenga upya Gaza.”

Ikiwa sifa za Trump kwa Erdogan zitaendelea, basi Ankara imepata fursa ya dhahabu kurejea katika meza ya maamuzi ya Mashariki ya Kati.

Kwa Washington, ni nadra kuona maelewano ya karibu kiasi hiki na mshirika wa NATO mwenye misimamo isiyoeleweka.

Lakini kwa Erdogan, huu ni ushahidi kwamba Uturuki, ambayo zamani ilitengwa kwenye diplomasia ya Kanda, sasa imerejea kama nguvu isiyoweza kupuuzwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *