Vyombo vya usalama vya Israel vimetangaza kuwa Hamas imekuwa ikiimarisha udhibiti wake katika Ukanda wa Ghaza tangu dakika za mwanzo za kusitishwa mapigano na inaendelea kurejesha utulivu na usalama katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo, licha ya uharibifu na jinai kubwa za miaka miwili zilizofanywa na utawala wa Kizayuni kwenye eneo hilo.

Shirika la Habari la Fars limelinukuu gazeti la lugha ya Kiebrania la “Haaretz” likiandika katika ripoti yake kwamba idara za usalama na kijasusi za utawala huo bado hazijaona dalili zozote za kuzuka vuguvugu la upinzani la wananchi au maandamano dhidi ya Hamas ambayo yangekwamisha udhibiti wa harakati hiyo katika Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa gazeti hilo la Kizayuni, tathmini zinaonesha kwamba makabila ya wenyeji ambayo Israel ilijaribu kuyaunga mkono wakati wa jinai zake huko Ghaza ili kuunda tishio la kisiasa na kijeshi kwa Hamas ima yamesambaratika au wanachama wao wamepata pigo ambalo limewazuia kuchukua hatua yoyote ya kushawishi wananchi waichukie na kuipinga Hamas.

Gazeti hilo limeongeza kuwa uchunguzi wa kiusalama unaonesha kuwa Hamas ilibakisha maelfu ya wanachama wake wakati wa vita kama kikosi cha akiba, ambao wote walikuwa na jukumu la kurejesha mara moja nguvu na udhibiti wa harakati hiyo kwenye Ukanda wa Ghaza na kurejesha utulivu na usalama baada ya kumalizika mapigano.

Amma kuhusu ujenzi mpya wa Ghaza, duru za Israel zinaamini kuwa Hamas inakabiliwa na matatizo katika ujenzi wa Ukanda wa Ghaza kwani inahitaji makumi ya mabilioni ya dola kuujenga upya ukanda huo. Hata hivyo harakati hiyo hivi sasa inafanya kazi ya kufungua tena barabara na mitaa na kukarabati miundombinu muhimu katika maandalizi ya kuanza tena maisha ya kawaida ya wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *