
Amechaguliwa kwa kura 237 katika bunge lenye viti 465. Chama cha Takaichi cha Liberal Democratic, LDP ambacho kimeiongoza Japan kwa muda mrefu, kimekubaliana kuunda serikali ya muungano na chama cha mrengo wa kulia cha Japan Innovation Party kijulikanacho kama Ishin.
Takaichi aliyekuwa msaidizi wa waziri mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe, alimuenzi sana waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Margaret Thatcher na anatarajiwa kurudi katika mtindo wa uongozi wa Abe wakati akijaribu kuufufua uchumi unaokuwa kwa kasi ndogo na kupambana na ongezeko la bei za bidhaa.
Huenda Takaichi pia akaipeleka Japan katika siasa za mrengo wa kulia hasa katika masuala ya uhamiaji na ulinzi, na kuwa kiongozi wa hivi karibuni kabisa kulipeleka taifa lake katika mkondo huo ambao siasa za dunia zinahamia.
Ushindi wake ni hatua muhimu katika nchi ambayo wanaume bado wana ushawishi mkubwa.