Takaichi anaingia madarakani katika kile wachambuzi wanakitaja kuwa mwelekeo mpya wa kisiasa kuelekea mrengo wa kulia nchini Japan. “Kulingana na Kifungu cha 18, Aya ya 2 ya Kanuni za Bunge la Wawakilishi, Sanae Takaichi anateuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Japan.” Ni maneno ya Spika wa Bunge la Japan Fukushiro Nukaga huku wabunge wakipiga makofi wakati Sanae Takaichi, mwenye umri wa miaka 64, alipothibitishwa rasmi kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo, na wa 104 kwa jumla.
Anachukua nafasi kutoka kwa kiongozi anayeondoka, Shigeru Ishiba, ambaye alijiuzulu kufuatia matokeo duni ya chama chake katika uchaguzi wa hivi karibuni.
Takaichi, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Liberal Democratic kinachotawala, alipata kura 237 kati ya viti 465 vya bunge la chini kabla ya kupata uungwaji mkono kama huo katika bunge la juu. Spika wa Bunge la Chini la Japan, Fukushiro Nukaga, ndiye aliyetangaza rasmi habari hiyo ya kihistoria.
Kupanda kwa Takaichi kunatokana na makubaliano ya dakika za mwisho ya kuunda muungano kati ya Chama cha Liberal Democratic, ambacho kimetawala siasa za Japan kwa miongo kadhaa, na Chama cha mrengo wa kulia cha Japan Innovation kinachojulikana kama Ishin.
Kwa pamoja, vyama hivyo viwili havina wingi wa kutosha bungeni, jambo linalomaanisha kuwa kiongozi huyo mpya atalazimika kushirikiana na upande wa upinzani ili kupitisha miswada muhimu.
Takaichi, ambaye ni mwanafunzi wa kisiasa wa marehemu Shinzo Abe na shabiki mkubwa wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher, anatarajiwa kufufua sera za Abenomics, zinazozingatia matumizi makubwa ya serikali na upatikanaji rahisi wa fedha, ili kufufua uchumi wa Japan unaodorora.
Hata hivyo, baadhi ya raia wanasema wana matumaini kuwa uongozi wake utaleta mabadiliko mazuri. Mao Mayimoto ni mwanamke anaefanya kazi ya mauzo mwenye umri wa miaka 29. ”Nilipomuona kwenye televisheni, nilihisi kwamba ni mtu mwenye nguvu na ushawishi mkubwa. Kulikuwa pia na utata kuhusu kauli yake ya ‘kazi, kazi, kazi,’ lakini ilionyesha wazi jinsi alivyo na ari na motisha kubwa.”
Takaichi anakabiliwa na jukumu gumu kufufua uchumi unaolemewa na mfumuko wa bei na deni la taifa, huku akijaribu kurejesha imani ya wapiga kura baada ya miaka kadhaa ya kashfa za kisiasa.
Ameahidi kuongeza matumizi ya ulinzi na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama kati ya Japan na Marekani, sera ambazo zinaweza kubadilisha utambulisho wa Japan kama taifa lenye msimamo wa upole baada ya vita.
Baraza lake la mawaziri, litakalotangazwa baadaye leo, linatarajiwa kujumuisha mwandani mwingine wa marehemu Shinzo Abe, Satsuki Katayama ambaye atakuwa waziri wa fedha wa kwanza mwanamke katika historia ya Japan.