Paris. Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, ameanza rasmi kutumikia kifungo chake cha miaka mitano gerezani, akiwa ameambatana na picha za familia na riwaya ya Alexandre Dumas ‘The Count of Monte Cristo’, inayoelezea maisha ya mtu asiye na hatia anayehukumiwa kifungo, kisha kutoroka na kulipiza kisasi.
Sarkozy ameingia gerezani mjini Paris leo Jumanne Oktoba 21, 2025 baada ya mahakama kumuhukumu kifungo cha miaka mitano kwa kosa la njama ya kihalifu, kuhusiana na mpango wa kupata fedha za kampeni za uchaguzi kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi.
Sarkozy, ambaye alikuwa rais wa Ufaransa kati ya mwaka 2007 na 2012, ndiye mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhukumiwa kifungo cha gerezani, na pia ni kiongozi wa kwanza wa Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia kufungwa jela.

Muonekano wa juu wa gereza la La Sante. Picha na Mtandao
Sarkozy aliliambia gazeti la Le Figaro la Ufaransa kuwa amebeba picha za familia na vitabu vitatu, kama alivyoruhusiwa kwa wiki ya kwanza kikiwemo kitabu kuhusiana na Yesu na riwaya ya Alexandre Dumas kuhusu mtu asiye na hatia anayehukumiwa kifungo gerezani kisha kutoroka na kulipiza kisasi.
Pia, atatumia muda wake gerezani kuandika kitabu ambacho hakusema kitahusu nini.
Sarkozy anatarajiwa kuwekwa selo ya peke yake kwa ajili ya usalama wake, katika chumba cha takriban mita za mraba tisa, chenye bafu na choo chake binafsi.
Hatakuwa na simu ya mkononi, lakini atakuwa na luninga ndogo.
Pia, ataruhusiwa kutumia simu maalumu inayodhibitiwa na ulinzi kuwasiliana na mawakili wake na familia.
Anatarajiwa kuruhusiwa kupokea wageni mara mbili kwa wiki kutoka kwa familia.
Pia, aliliambia gazeti la Le Figaro kuwa alishauriwa kubeba vifaa vya kuziba masikio. “Usiku unasikia kelele nyingi, watu wakipiga mayowe, wakilalamika,” alisema.

Muonekano wa moja ya chumba cha gereza la La Sante. Picha na Mtandao
Sarkozy ndiye kiongozi wa kwanza wa Ufaransa kufungwa jela tangu Philippe Pétain, kibaraka wa Wanazi ambaye alihukumiwa kifungo gerezani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Chama cha wafanyakazi wa magereza kilifanya maandamano nje ya gereza hilo kupinga msongamano mkubwa wa wafungwa katika magereza ya Ufaransa, ambapo wafungwa wengi wanalazimika kulala kwenye magodoro yaliyowekwa sakafuni hali tofauti kabisa na ile anayopata Sarkozy.
Alivyosindikizwa jela na familia
Sarkozy, ambaye tayari amekata rufaa kupinga hukumu hiyo, alijaribu kuepuka kupigwa picha akiwa langoni mwa gereza la La Santé kusini mwa Paris.
Badala yake, alipanga kwa makini kuondoka nyumbani kwake magharibi mwa jiji hilo, ambapo alitembea pamoja na mkewe, mwanamuziki Carla Bruni huku akisalimiana na watu waliokusanyika mitaani.
Kwanza, watoto wake wakiongozwa na Giulia, binti yake mwenye umri wa miaka 14 aliyempata na Bruni, walitembea polepole kutoka nyumbani wakisalimia watu waliokuja kumtakia kheri.

Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy akiwa na mkewe Carla Bruni, wakati akienda kuanza maisha mapya ya miaka mitano gerezani.
Louis Sarkozy, mmoja wa wanawe, ambaye anajiandaa kugombea nafasi ya meya mjini Menton kwenye pwani ya Ufaransa msimu ujao, alikuwa amewataka wafuasi wake waandamane mitaani.
Baadhi yao walikuwa wakipiga kelele: “Nicolas! Nicolas!” Wakati huohuo, akaunti ya Sarkozy ya mitandao ya kijamii ilichapisha ujumbe uliosema: “Mimi sina hatia”, na kwamba kifungo chake ni ‘kashfa ya kimahakama’.
Sarkozy alikutwa na hatia mwezi uliopita kwa kosa kuhusiana na mpango wa kutafuta ufadhili kutoka kwa utawala wa Gaddafi kwa ajili ya kampeni yake ya uchaguzi wa urais wa Ufaransa ya mwaka 2007, na alishinda uchaguzi huo.
Kiongozi wa jopo la majaji katika kesi hiyo, Jaji Nathalie Gavarino, katika hukumu yake alieleza kesi hiyo ilikuwa na ‘uzito wa kipekee’ na ‘ingeweza kuathiri imani ya raia’.

Gari lililombeba Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, likiwasili katika gereza la La Santé, Paris, Ufaransa, leo Oktoba 21, 2025.
Hata hivyo, mawakili wa Sarkozy waliwasilisha ombi la kuachiwa huru mara tu alipoingia gerezani, na mahakama ya rufaa ina miezi miwili kuchunguza ombi hilo.
Kesi ilivyokuwa
Wakati wa kesi hiyo iliyodumu kwa miezi mitatu, mwendesha mashtaka wa umma aliieleza mahakama kuwa Sarkozy aliingia kwenye ‘mkataba wa kishetani wa rushwa’ na mmoja wa madikteta wa kutisha zaidi wa miaka 30 iliyopita ili kupata fedha za kampeni kutoka kwa Gaddafi.

Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy (kushoto) akisalimiana na kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Sarkozy aliachiliwa huru katika mashtaka mengine matatu tofauti: ya rushwa, matumizi mabaya ya fedha za umma za Libya, na ufadhili haramu wa kampeni za uchaguzi.
Katika kesi hiyo, Sarkozy alikana makosa na kusema kuwa hakuwa sehemu ya njama yoyote ya kihalifu ya kutafuta fedha kutoka Libya.
Wasemavyo watu
Watu sita kati ya 10 nchini Ufaransa wanaamini kuwa kifungo cha Sarkozy ni ‘cha haki’, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni ya kura ya maoni ya Elabe, uliowashirikisha zaidi ya watu wazima 1,000.

Carla Bruni-Sarkozy na watoto wake akimuaga mumewe Sarkozy wakati anaenda gerezani kutumikia kifungo jela
Hata hivyo, Sarkozy bado anaungwa mkono na watu wa mrengo wa kulia nchini Ufaransa.
Rais Macron amkaribisha ikulu
Taarifa zingine zinaeleza Rais Emmanuel Macron alimkaribisha Sarkozy katika Ikulu ya Élysée siku ya Ijumaa.
“Kwa upande wa kibinadamu, ilikuwa ni kawaida kumpokea mmoja wa watangulizi wangu katika hali hii,” Macron aliwaambia waandishi wa habari.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron (kulia) akiwa na Nicolas Sarkozy. Picha na Mtandao
Hata hivyo, kiongozi wa chama cha Kisoshalisti, Olivier Faure, alimkosoa Macron kwa kumwalika Sarkozy Élysée kabla hajaingia gerezani.
“Hii ni aina ya shinikizo kwa mfumo wa haki. Inatoa hisia kwamba kuna washtakiwa ambao kwa asili ni tofauti na wengine,” alisema.
Waziri wa haki, Gérald Darmanin, ambaye ni mfuasi wa kisiasa wa Sarkozy, alisema atamtembelea Sarkozy gerezani katika wadhifa wake wa uwaziri.
Baadhi ya wafungwa maarufu waliowahi kufungwa katika gereza la La Santé, wakiwemo wapiganaji kama Ilich Ramírez Sánchez kutoka Venezuela, anayefahamika pia kama Carlos the Jackal, ambaye kwa sasa amehamishiwa gereza lingine.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao