
Kibaha. Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani, yameingia katika hatua ya mwisho, huku vifaa vyote vya kupigia kura vikiwa vimepokelewa rasmi kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Oktoba 21, 2025 Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kibaha Mjini, Theresia Kyara amesema maandalizi yote yanaendelea vizuri kuelekea siku ya upigaji kura itakayofanyika Oktoba 29, 2025 nchi nzima.
“Tayari tumepokea vifaa vyote vitakavyotumika kupigia kura kutoka Tume Huru ya Uchaguzi, na tunatarajia kuanza kutoa mafunzo kwa wasimamizi na makarani wa vituo kuanzia Oktoba 25,” amesema Kyara.
Amesema jumla ya wapiga kura waliojiandikisha katika Jimbo la Kibaha Mjini ni 188,659, kutoka tarafa mbili, kata 14 na vituo vya kupigia kura 467.
Amefafanua kuwa mafunzo kwa makarani yataanza Oktoba 25, huku wasimamizi wa vituo wakipewa mafunzo maalum kwa siku mbili, Oktoba 26 na 27, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa weledi na ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Kibaha, Mwita Magige amewataka walimu kujitokeza kushiriki uchaguzi huo kwa amani na kutimiza haki yao ya kikatiba.
“Kwa wale walimu walioteuliwa kusimamia uchaguzi, ni muhimu kufanya kazi hiyo kwa uadilifu, uaminifu na kufuata taratibu zilizowekwa, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na utulivu,” amesema Magige.
Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wa Kibaha, akiwemo Nuru Joseph na Naomi Mkonyi, waliwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji na vitisho vinavyodaiwa kusambazwa kuhusu uwepo wa maandamano siku ya uchaguzi.
“Tunaomba watu waache maneno ya vitisho. Kaeni mtulie, mjitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani. Vitisho vinakatisha tamaa wapiga kura,” wamesema wananchi hao.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, ambapo wananchi watapiga kura kuwachagua viongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais.