gen z

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika miezi ya hivi karibuni, dunia imeendelea kushuhudia maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana ‘Gen-Z’.

Kutoka Asia Kusini, kusini mashariki mwa Asia, barani Ulaya hadi Afrika Mashariki, nguvu za kizazi cha sasa cha vijana ‘Generation Z’ zimekuwa zikitikisa tawala na kuibua mijadala kuhusu haki za kijamii, nafasi ya vijana katika siasa, na mustakabali wa uchumi.

Tofauti na vizazi vilivyotangulia, Gen Z imekua katika mazingira ya kidijitali ambapo mitandao ya kijamii ni chombo cha uratibu na sauti ya pamoja.

Ndani ya mwaka 2025 pekee, kuanzia Januari hadi Septemba, maandamano yaliyopangwa na kizazi hiki yamekuwa yakionekana mara kwa mara, yakisababisha hata kujiuzulu kwa viongozi, kusitishwa kwa sera na kuibuka kwa mijadala mipya ya kitaifa.

Lakini kinachojitokeza ni swali kubwa: vijana hawa wanapigania nini hasa, na je, maandamano haya yana nafasi ya kuleta mabadiliko ya kudumu?

Nchi za hivi karibuni kuandamana

Mwezi Oktoba, Madagascar, Peru na Morocco, maandamano ya Gen Z yalikuwa na nguvu kubwa, yakileta matokeo Madagascar, Morocco yakiendelea kwa kasi.

Katika mwezi wa Septemba pekee, Nepal iligeuka kitovu cha vuguvugu la Gen Z baada ya serikali kuzuia majukwaa kadhaa ya mitandao ya kijamii. Marufuku hayo yalichukuliwa kama jaribio la kunyamazisha sauti za wakosoaji, na vijana wa kati ya miaka 18 hadi 28 walimiminika mitaani kwa wiki nzima. Takriban watu 70 waliuawa katika ghasia zilizofuatia, na hatimaye Waziri Mkuu K.P. Sharma Oli alilazimika kujiuzulu.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa Ufilipino, ambapo tarehe 21 Septemba maelfu ya vijana waliandamana katika mji mkuu Manila wakipinga kile walichokitaja kuwa ufisadi wa kimfumo na matumizi mabaya ya fedha za umma. Waandamanaji, wengi wao wakiwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wahitimu wachanga, walisema hawawezi kukaa kimya wakati mustakabali wao unakumbwa na ufisadi na ukosefu wa fursa.

Ukiancha indonesia pia huko Mongolia, maandamano ya Mei 2025 yaliibua upinzani mkubwa dhidi ya matumizi ya kifahari ya serikali. Vijana waliokuwa mstari wa mbele waliitaka serikali iwajibike kwa kushindwa kudhibiti ufisadi.

Huko Timor-Leste, maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi mnamo Septemba yalilazimisha serikali kusitisha mpango wa kununua magari ya kifahari kwa wabunge, hatua iliyokuwa ishara ya ushindi mdogo kwa vijana wa nchi hiyo.

Barani Ulaya, Ufaransa iliendelea kushuhudia maandamano dhidi ya mageuzi ya pensheni na gharama ya maisha, ambapo makundi ya vijana walijiunga na vyama vya wafanyakazi kushinikiza serikali kurejelea sera zake.

Afrika Mashariki nayo haijabaki nyuma. Nchini Kenya, maandamano makubwa ya kizazi kipya yalitikisa taifa hilo mwaka 2024 na kuendelea mwaka huu, yakilenga haswa hali ya maisha na uwajibikaji wa viongozi kwa makosa yakiwemo ya mauaji.

Na kwa upande wa Tanzania, makundi ya vijana tayari yametangaza mipango ya kuandamana tarehe 29 Oktoba, siku ya uchaguzi, wakitaka mabadiliko na kusikika kwa sauti zao katika mustakabali wa taifa.

Kwanini wanaandamana, wanataka nini?

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Sababu kuu zinazowaunganisha vijana hawa ni ufisadi, gharama kubwa ya maisha, ukosefu wa ajira na kudorora kwa nafasi ya kizazi kipya katika siasa za kitaifa. Katika nchini ya Nepal kwa mfano, maandamano yaliibuka si tu kutokana na marufuku ya mitandao ya kijamii, bali pia kutokana na hasira dhidi ya kile kilichoitwa utawala wa watoto wa wakubwa, ambapo familia za kisiasa zimekuwa zikidhibiti nafasi za mamlaka kwa vizazi kadhaa na zimekuwa zikijinufaisha.

Harakati ya #NepoBabies ilitumika kama alama ya upinzani huo, ikisisitiza kwamba vijana wa kawaida wanazuiwa kupata nafasi sawa.

Ufilipino ilishuhudia sauti zinazopinga rushwa iliyodumu kwa miongo kadhaa, ambapo waandamanaji walihusisha moja kwa moja matatizo ya mafuriko na majanga ya asili na miradi ya serikali iliyokumbwa na ufisadi.

Timor-Leste, kwa upande mwingine, maandamano yalihusu matumizi mabaya ya bajeti ya umma katika kununua magari badala ya kuwekeza kwenye elimu na huduma muhimu.

Huko Ufaransa, maandamano ya vijana yalichochewa na mageuzi ya pensheni na gharama ya maisha, wakihisi kuwa kizazi chao kinabeba mzigo wa sera zisizo na tija huku wakikosa hakikisho la maisha bora ya baadaye. Barani Afrika, maandamano ya Kenya yalilenga kupinga ongezeko la kodi na hatua za kiuchumi ambazo vijana walihisi zinawakandamiza zaidi, baadaye kulikuja sababy ya mauaji kama ya Albert Ojwang, huku Tanzania sasa ikielekea kwenye mtihani wake wakati wa uchaguzi wa Oktoba.

Maandamano yatafanikiwa?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kiwango cha mafanikio ya maandamano haya kinabaki kuwa mjadala wazi. Nepal imetoa mfano dhahiri wa jinsi shinikizo la barabarani linaweza kuibua mabadiliko ya moja kwa moja, kwa kuwa waziri mkuu alilazimika kuachia madaraka.

Kanali Michael Randrianirina ameapishwa kuwa Rais mpya wa Madagascar katika kumrithi Andry Rajoelina, rais wa zamani aliyeikimbia nchi na baadaye kuondolewa madarakani kufuatia maandamano ya kudai uwajibikaji zaidi.

Timor-Leste pia ilionyesha ushindi wa haraka pale ambapo serikali ilisitisha mpango wake wa manunuzi baada ya shinikizo la wanafunzi. Hata hivyo, katika nchi nyingi, maandamano haya bado yamekumbwa na changamoto kubwa, ikiwemo ukandamizaji wa polisi, kukamatwa kwa viongozi wa wanafunzi na ukosefu wa uratibu thabiti wa kisiasa.

Wachambuzi wanasema kwamba nguvu ya Gen Z iko katika mshikamano na ubunifu wao wa kidijitali, lakini changamoto kubwa ni kugeuza nguvu za barabarani kuwa mabadiliko ya kudumu ya sera. Maandamano yanapoweza kulazimisha kujiuzulu kwa waziri au kufutwa kwa sera, bado yanakosa miundombinu ya kisiasa ya kushinikiza mabadiliko ya kina.

“Maandamano haya yamebadili mtazamo wa wengi wanaelewa umuhimu wa kutetea haki zao na kutonyamaza kwani mabadiliko hayapatikani kwa kukaa kimya,” alisema Hussein Khalid, Mwaharakati na Afisa Mkuu wa Shirika la Vocal Afrika wakati wa maandamano ya Kenya.

Maandamano mengi yalifanikiwa kwa kutumia teknolojia ya mitandao ya kijamii na hili sio jambo jipya. Mwanzoni mwa miaka ya 2000 utumaji ujumbe mfupi wa maandishi ulichochea mapinduzi ya pili ya nguvu ya watu nchini Ufilipino. Aidha wakati Arab Spring na Occupy Wall Street katika miaka ya 2010 maandamano yalichochewa sana na mitandao ya Twitter ambayo sasa inaitwa mtandao wa X.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba sauti ya Gen Z haiwezi tena kupuuzwa. Kila nchi inayoshuhudia maandamano haya inakumbushwa kuwa kizazi kipya kina matarajio makubwa zaidi ya uwajibikaji na usawa. Swali ambalo halina jibu la moja kwa moja ni iwapo sauti hizi zitasababisha mageuzi ya kudumu au zitabaki kuwa alama za upinzani wa kizazi kilichochoshwa na mifumo ya zamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *