KOCHA wa Nsingizini Hotspurs, Mandla Qhogi, ameonyesha imani kwa kikosi chake licha ya kupoteza kwa mabao 3–0 dhidi ya Simba katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa King Sobhuza II Memorial, Eswatini, Oktoba 19, 2025.
Akizungumza kabla ya safari ya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya marudiano, Qhogi amesema bado anaamini kikosi hicho kina uwezo wa kufanya maajabu, akisisitiza mpira wa miguu una matokeo yasiyotabirika na kwamba watatua Tanzania wakiwa na dhamira moja tu – kupambana hadi dakika ya mwisho.
“Hatuwezi kuiangusha nchi. Mchezo huu una maana kubwa kwetu na kwa taifa. Tunahitaji kuonyesha uzalendo, nidhamu na ari ya kupambana. Hatujakata tamaa, tunaamini bado inawezekana kufanya kitu kikubwa,” amesema Qhogi.
Kocha huyo amesema haoni tofauti kubwa ya kucheza nyumbani au ugenini, akisema kinachotakiwa zaidi ni umoja na utulivu wa akili.

“Haijalishi tunacheza nyumbani au ugenini, kilicho muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja. Timu yetu imekuwa ikijifunza kupitia makosa na tunaamini tutajituma zaidi katika mechi ya marudiano,” ameongeza.

Licha ya matokeo mabaya katika mechi ya kwanza, Qhogi amesema amekuwa akijaribu kuwapa wachezaji wake motisha kubwa ya kuamini katika uwezo wao, akiamini kwamba mechi ya Dar es Salaam inaweza kutoa matokeo tofauti.
“Tumezungumza nao, tumejaribu kuwaweka sawa kisaikolojia. Tunawaambia waamini kwamba bado inawezekana hata tukicheza ugenini. Kama wao walipata mabao matatu kwetu basi hata sisi inawezekana kwao,” amesema.

Katika mahojiano mengine, Qhogi amezungumzia hali ya baadhi ya wachezaji wake, akimtaja kiungo Sambulo Masoso Simelane kuwa bado hajarejea katika ubora wake, huku akiahidi kumpa muda kurejea katika hali ya kawaida.
“Masoso si yule tuliyemzoea, amekuwa akipoteza kasi kutokana na uzito alioongeza. Tunampa muda arejee katika hali yake ya kawaida kwa sababu ni mchezaji muhimu kwenye mipango yetu,” amesema Qhogi.

Qhogi, ambaye anaonekana kuwa na matumaini ya kupindua meza jijini Dar es Salaam, amesema mechi dhidi ya Simba ni changamoto kubwa.
“Tunajua ukubwa wa Simba na uzoefu wao katika michuano ya Afrika, lakini hilo halitupi hofu. Tunataka kuonyesha dunia kwamba Nsingizini inaweza kushindana,” amesema.

Mechi hiyo ya marudiano kati ya Simba na Nsingizini Hotspurs inatarajiwa kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku Simba ikiwa na nafasi kubwa ya kutinga hatua ya makundi kufuatia mtaji wa mabao matatu ilioupata Eswatini wikiendi iliyopita chini ya meneja, Dimitar Pantev.
Ili kufuzu hatua ya makundi, Nsingizini inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao angalau 4-0, kinyume na hapo safari yao inakuwa imefika mwisho. Simba yenyewe kazi imebaki kulinda ushindi huo ili kufuzu makundi.