Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kukamilisha miradi mikubwa itakayoongeza kasi ya biashara na kukuza uchumi wa Jiji la Dar es Salaam, ukiwamo wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), iwapo atachaguliwa kuendelea kuongoza nchi kwa kipindi kijacho.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 21, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Leaders Club, Samia ameahidi kuwa Serikali yake itaendelea kuboresha miundombinu ya jiji hilo kwa kujenga madaraja ya juu (flyovers) na kuboresha barabara kuu zenye msongamano mkubwa.

Amesema miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la juu kutoka Morocco–Mwenge hadi Magomeni, pamoja na barabara za Ali Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa, ili kupunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi katika shughuli za biashara.
Mradi wa BRT
Samia amesema sekta binafsi imeanza kutoa huduma za usafiri kupitia mradi wa BRT, ambao ujenzi wake umefikia asilimia 61 na tayari kilomita 94.9 za barabara zimekamilika, huku Sh2.1 trilioni zikiwa zimetumika.
Ameahidi akipata ridhaa ya wananchi, Serikali yake itahakikisha awamu zote za mradi huo zinakamilika na kuendeshwa kwa ufanisi na sekta binafsi.
“Sekta binafsi wataendesha mabasi hayo kwa kupakia abiria. Kampuni ya ENG imeingiza mabasi 177, YG Link mabasi 166, Metro City mabasi 334, na Mofat mabasi 255 ambayo yako njiani. Kuanzia Januari 2026 mtaona mageuzi makubwa katika huduma za mabasi ya mwendokasi,” amesema Samia.
Ameongeza kuwa mradi huo unaipa Tanzania sifa kimataifa kwa ubora wa uwekezaji wake na utakuwa chachu ya mageuzi makubwa katika usafiri wa jiji hilo.
Miundombinu ya barabara
Kuhusu uboreshaji wa barabara, mgombea urais huyo amesema anatambua changamoto za uchakavu na uharibifu wa miundombinu kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa nyakati tofauti na kwamba, Serikali itakamilisha barabara zote zilizoko katika hatua za ujenzi.
Amezitaja baadhi ya barabara hizo kuwa ni Kimara–Mavurunza–Bunyokwa–Kinyerezi yenye urefu wa kilomita saba, inayopita katika majimbo ya Segerea, Kibamba na Ubungo. Amesema pia Serikali itaongeza bajeti kwa ajili ya barabara mpya zitakazokuza maendeleo ya jiji hilo.
“Tutapanua barabara ya Mwai Kibaki (Morocco–Kawe) yenye urefu wa kilomita tisa na barabara ya Tegeta–Bagamoyo yenye urefu wa kilomita 57,” amesema Samia.
Kwa Jimbo la Ubungo, mgombea huyo ameahidi kukamilisha barabara ya Kibamba–Mloganzila yenye urefu wa kilomita nane, sambamba na kuboresha barabara za ndani.
Akizungumzia mafuriko, Samia amesema Serikali yake itatatua tatizo la mafuriko katika maeneo yanayopakana na Mto Gide, Mto Mbezi na Mto China kupitia Awamu ya Pili ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), pamoja na kuboresha mifereji ya maji katika maeneo ya Magomeni, Tandale na Makumbusho.
Kwa upande wa usafiri wa daladala, Samia amesema Serikali itakamilisha ukarabati wa stendi za Mwenge, Kawe, Bunju B na Tegeta Nyuki, ili ziwe na miundombinu bora na mpangilio wa safari.
Miradi ya maji
Mgombea urais Samia ameahidi kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji itakayohudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, ikiwamo mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji unaolenga kumaliza tatizo la maji hasa wakati wa kiangazi.
Aidha, amesema Serikali itaharakisha kukamilika kwa bwawa la Kidunda lenye thamani ya Sh336 bilioni litakalosaidia kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama.

“Mradi wa Rufiji tumeanza kwa upembuzi yakinifu na utafiti wa kina. Awamu hii tutaanza utekelezaji ili Dar es Salaam ipate maji ya uhakika kutoka Kidunda, Ruvu na Rufiji,” amesema.
Mkoa wa Dar es Salaam nao unakabiliwa na migogoro ya ardhi, hivyo,Samia ameahidi kufanyia kazi kero hiyo akipatiwa ridhaa Jumatano Oktoba 29, 2025.
Amesema migogoro hiyo imekuwa changamoto kubwa, kwa sababu kiwanja kimoja huuzwa kwa watu zaidi ya wanne, hususan katika maeneo ya Mabwepande, Mbweni, Bunju, Madale na Nyakasangwe.
Amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuratibu, kurasimisha na kutatua migogoro hiyo kupitia ofisi za mkoa na wilaya.
Amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba za viwango tofauti jijini humo na Serikali ya CCM itatekeleza mpango maalum wa ‘Mama Samia Housing’ utakaolenga kupunguza uhaba wa makazi bora kwa wananchi.
Aonya juu ya maandamano
Akizungumzia hoja za maandamano, Samia ambaye pia ni Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, amesema maandamano yatakayofanyika Oktoba 29, 2025 ni ya kwenda kwenye vituo vya kupiga kura, huku akiwataka Watanzania kumwachia matusi kwa kuwa anayabeba kwa niaba yao.
Amesema Watanzania wawe na amani kwa kuwa hakuna tishio la kiusalama litakalotokea siku ya uchaguzi mkuu na amewaomba wakichague Chama cha Mapinduzi.
“Niwahakikishie kuwa Oktoba 29, 2025 kesho kutwa, tokeni muende mkapige kura, ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii. Nataka niwaambie maandamano yatakayokuwepo ni watu kwenda vituoni kupiga kura, hakuna maandamano mengine yatakuwepo, hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo, anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi,” amesema.
Ameongeza: “Niwaombe ndugu zangu twendeni tukapige kura, baba ukitoka hakikisha unatoka na familia nzima kila aliyeandikishwa. Mabalozi wetu tokeni na watu wenu wote mkapige kura, twendeni mkaheshimishe CCM, tukaiheshimishe Tanzania tukapige kura kwa usalama turudi kwa usalama.”
Amesema aliapa kutumikia Tanzania na ndicho anachokifanya, aliapa kulinda nchi, kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha na kuwa anapohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wanapata elimu na huduma zingine na kuhakikisha usalama wa nchi upo ndiyo kuheshimisha utu wa Mtanzania.
“Ndugu zangu, mengine niachieni mimi, matusi niachieni mimi, nayabeba kwa niaba yenu manabii wetu Bwana Yesu alisulubiwa kwa kukomboa watu kwa ajili ya Mungu, lakini alikuwa anakomboa watu. Muhammad alipigwa mpaka akatolewa meno kwa kufanya kazi ya kukomboa watu kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
“Samia Suluhu aliapa kuitumikia Tanzania na ndicho ninachokifanya, niliapa kulinda nchi na ndicho ninachokifanya, niliapa kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha utu wa Mtanzania, ndicho ninachokifanya. Ninapohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wetu wanapata elimu umeme upo, usalama wa nchi upo, ni kuheshimisha utu wa Mtanzania,” amesema.
Amesisitiza kwamba hana uchungu kubeba kubeba matusi yote yanayotolewa kwa sababu anafanya kazi hiyo, hana uchungu hata kidogo wala hajutii, kwa hiyo amewaomba kura wananchi wa Ubungo na Kinondoni,” amehitimisha mgombea huyo
Kauli za wagombea
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa Jimbo la Mkuranga, ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema Serikali ya Samia imetoa zaidi ya Sh1.7 trilioni katika miradi ya kupunguza msongamano na mafuriko jijini Dar es Salaam.
“Ulitupa maagizo mawili, kuondoa msongamano na kupunguza mafuriko. Fedha hizo zimetolewa, na hii inaonyesha utu wako kwa kugusa maisha ya Watanzania,” amesema Ulega.
Naye Mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inayoongozwa na Samia imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya biashara jijini Dar es Salaam kwa kuondoa kodi zisizo za haki zilizokuwa zikiwalemea wafanyabiashara.
“Uliposema hutaki serikali iendeshe nchi kwa mapato ya dhuluma, ulirudisha imani ya wafanyabiashara wa jiji hili,” amesema Nchemba.
Awali, Ezekiah Wenje aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria na sasa mwanachama wa CCM, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kumchagua Samia Suluhu Hassan na CCM.

Wenje amepongeza ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 kwa kujumuisha mpango wa kuendeleza mchakato wa katiba mpya, akibainisha kuwa ucheleweshaji wa awali ulisababishwa na wapinzani waliokimbia Bunge la Katiba.
“Sisi wapinzani tulichelewesha upatikanaji wa katiba mpya tulipokimbia Bunge la Katiba la Warioba. Hata mchakato ukianza tena, naamini bado watakimbia,” amesema Wenje.