LICHA ya kwamba huku mtaani mashabiki wa Yanga hawana furaha, lakini mastaa wa kikosi hicho wanawataka wasihofu, kwani wale Silver Strikers hawatoki kwa Mkapa, Jumamosi wiki hii.
Na katika kuhakikisha kwamba hilo linatimia unaambiwa kwamba tizi linalopigwa kambini kwao kule Avic, Kigamboni, Dar es Salaam si mchezo, huku mzuka ukiwa bab’kubwa.
Lakini katika kusherehesha hilo baadhi ya wachezaji wamezungumzia mikakati ya mechi hiyo ya Jumamosi wakisema wameyachukua matokeo ya kupoteza ugenini, ila msimamo wao ni kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufanya vizuri nyumbani.

Kiungo wa timu hiyo, Pacome Zouzoua ameambia Mwanaspoti kuwa baada ya mchezo huo wa kwanza matokeo hayo yaliwaumiza lakini wamejipanga kulipa kisasi na kwamba, Wamalawi hao hawataamini.
Zouzoua amesema hawana sababu ya kuendelea kuinamisha vichwa chini, badala yake wanataka kurudisha furaha ya mashabiki wao kwa kushinda kwa kuwa wana timu kubwa inayoweza kutengeneza matokeo kokote.
“Kila mmoja ameumizwa na yale matokeo, wote kwenye timu tulikuwa kama tumepata taarifa mbaya ambayo hatukuitarajia, tumejua wapi tulikosea na tutarekebisha.
“Walishinda kwao na sisi tunarudi nyumbani tutakuwa mbele ya mashabiki wetu, tunataka kurudisha heshima ya klabu hii na furaha ya mashabiki wetu, tunataka kushinda ili twende makundi,” amesema kiungo huyo raia wa Ivory Coast.
Naye nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job amesema: “Tumeteleza kwenye mchezo wa kwanza, tulianza vizuri kipindi cha kwanza, kosa letu kubwa hatukutumia nafasi na wao wakaja kutumia nafasi moja waliyoipata kipindi cha pili.

“Tumeumizwa lakini tumejifunza na hata tulipokutana tumekubaliana tunarudi nyumbani kubadilisha, hii ni timu ambayo tumewahi kushinda pale ambapo ilionekana hatutaweza kushinda, tulifanya ugenini na hata nyumbani tunakwenda kufanya kweli, tunawaomba mashabiki wasikate tamaa waje uwanjani.”