Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema kuanzia Januari mwaka 2026, wakazi wa Dar es Salaam, watashuhudia mageuzi ya huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Amesisitiza dhamira ya Serikali yake ni kuhakikisha mradi huo, unaendelea kuipa sifa Tanzania kimataifa, hivyo sekta binafsi itapewa kipaumbele kuendelea kutoa huduma za mabasi hayo.
Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumanne Oktoba 21, 2025 alipozungumza na wananchi wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam katika mikutano yake ya kampeni za urais.
“Ahadi yetu kwenu ni kuanzia Januari mwaka 2026, wakazi Dar es Salaam mtaanza kuona mageuzi makubwa kwenye utoaji huduma ya miundombinu ya barabara za mwendokasi,” amesema.
Ameeleza hatua iliyofikia sasa katika mradi huo, imejenga sifa kimataifa, hivyo sifa iliyopo itaendelea kulindwa na mradi utaleta mapinduzi kwenye usafiri ndani ya Dar es Salaam.
Katika kipindi cha awamu ya sita, amesema kilomita 99.6 za barabara za mabasi hayo zimejengwa na kukamilika kwa asilimia 61, uliogharimu Sh2.1 trilioni zimetumika.
Ameahidi kujenga awamu zote za mradi na kuzikamilisha na kusimamia ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi ili kuipa sekta hiyo fursa zaidi.
Amesema tayari wameshapatikana watoa huduma katika awamu ya kwanza ambaye ni kampuni ya ENG yenye mabasi 177 na tayari yameanza kutumika.
“Awamu ya pili kampuni ya Mofat yenye mabasi 255 na mabasi ya Mofat tayari yameingia njiani,” amesema.
Katika awamu ya tatu, amesema Kampuni ya YG Link imeshapatikana na itakuwa na mabasi 266 na yatatumika pale awamu hiyo itakapokamilika.
Kwa awamu inayofuata, amesema Kampuni ya Metrolink City yenye mabasi 334 nayo itaingia kutoa huduma.
#StarTvUpdate