Ikiwa imetimia miaka 32 baada ya rais wa kwanza wa Burundi Melchior Ndadaye kuuwawa yeye pamoja na washirika wake wa karibu mnamo Oktoba 21 mwaka 1993, shirika la AVOD lililoanzishwa na wajane na yatima wa wahanga wa mauwaji hayo wameitaka serikali ya Rais Evariste Ndayishimiye kuhakikisha kuwa hukumu ya kesi hiyo inatolewa na ukweli unawekwa wazi. Pia shirika hilo limeitaka serikali kuwapatia hadhi ya kitaifa na kufikiria kuwalipa fidia.

Tamko rasmi la shirika hilo la wajane na yatima wa mauaji hayo, mbali na kupongeza hatua ya hayati Melchior Ndadaye ambaye alichaguliwa kidemokrasia na kupewa hadhi kama kinara wa demokrasia, wameitaka serikali kuhakikisha kwamba kesi inayowakabili waliohusika na mauwaji hayo inamalizika na hukumu inatolewa dhidi yao.

Setuturu Emmanuel, kiongozi wa shirika hilo la AVOD, anasema shirika lao limeitaka serikali kufanya kila liwezekanalo ili kesi hiyo iweze kumalizika na ukweli upatikane. ”Shirika la AVOD, linalowajumuisha wajane na yatima wa mauwaji ya Oktoba 21 1993, linaitaka serikali kusimamia kesi ya waliohusika na mauwaji ya Melchior Ndadaye na washirika wake iweze kumalizika na ukweli ujulikane. Shirika la AVOD linaitaka pia serikali kuwapatia hadhi ya kitaifa wajane na yatima wa washirika wake Melchior Ndadaye.”

Askari wa Burundi wakishika doria kwenye mitaa ya Bujumbura wakati wa mazishi ya Ndadaye na maafisa wengine sita wa serikali.
Melchoir Ndadaye alikuwa rais wa kwanza wa Burundi aliyechaguliwa kutoka jamii ya Wahutu walio wengi.Picha: ALEXANDER JOE/AFP/Getty Images

Tamko la shirika hilo limetolewa wakati ambapo kesi hiyo imewekwa kwenye mchakato wa kitaifa wa kutafuta ukweli na maridhiano nchini Burundi.

Awali shirika hilo lilibainisha kuridhia mchakato huo, lakini kwanza walitaka wote waliotajwa na vyombo vya sheria kupanga na kuhusika na mauwaji hayo waombe radhi kwa familia za wahanga wa mauwaji hayo.

Ahishakiye Adela mjane wa aliyekuwa Spika wa Bunge kwenye utawala wa Rais Ndadaye anasema waliohusika na mauwaji hayo walitakiwa kujitokeza na kukiri makosa yao, na ikiwezekana walipe fidia.

Baada ya hukumu ya kesi hiyo kutangazwa, serikali kupitia wizara ya sheria ilikata rufaa kwa hoja kuwa waliohukumiwa ni wale waliotekeleza pekee mauaji hayo, huku waliopanga  mauwaji yaliyofuatia wakisalia bila kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hata hivyo, wengi ya wanaotajwa kupanga mauwaji yaliyogharimu maisha ya Rais Ndadaye na washirika wake wa karibu, akiwemo Rais wa zamani Pierre Buyoya walikwishafariki.

Ndadaye, aliiongoza nchi hiyo kwa siku 102, kabla ya kuuawa. Miaka 32 baada ya kutokea mauwaji hayo, hukumu ya mwisho ya kesi hiyo bado haijatolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *