Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay amerejea nchini akitokea Uholanzi alikokwenda kushiriki mashindano ya TCS Amsterdam Marathon 2025, ambapo amekiri kukutana na ugumu.

Mbio hizo zilifanyika Oktoba 19, 2025 ambapo Geay alimaliza wa nne kwa muda wa saa 2:04:36, huku Mkenya Geoffrey Toroitich Kipchumba akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kukimbia saa 2:03:30 na kuweka rekodi ya mwanariadha ambaye amekimbia muda mfupi zaidi katika mbio hizo.

Kwa kutumia saa 2:04:36, imemfanya Geay kujitengenezea muda wake bora kwa marathoni ambazo amekimbia mwaka huu ikiwemo Daegu za Korea Kusini na Berlin nchini Ujerumani, pia amefuzu mashindano makubwa ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na mashindano ya dunia.

Akizungumza na Mwanaspoti katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) muda mfupi baada ya kuwasili, Geay amesema mashindano yalikuwa magumu kutokana na aina ya wapinzani ambao walikuwepo, hivyo anamshukuru Mungu kwa kumaliza nafasi ya nne.

RIAD 01

“Nilifanya kadri ya uwezo wangu na nikashika nafasi ya nne, ambayo imenifanya kupata muda mzuri ambao ni bora kwangu mwaka huu.

“Mashindano ni magumu, waliopo pale ni washindani ambao kwa kweli wana ushindani mkubwa ambao mwenyewe sikutegemea,” amesema Geay.

Rogath John Stephen Akhwari ni Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), amesema wanajivunia kwa wanariadha wao kufanya vyema hasa kwa wikiendi iliyopita katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Amsterdam Marathon ambapo Geay alishika nafasi ya nne na kuweka muda wake bora kwa mwaka huu.

“Ni jambo la kishujaa ambalo Gabriel amefanya, tumeangalia yale mashindano, kuna wakati uliona mtangazaji wa mbio zile akisema sasa Tanzania imerudi, Gabriel Geay anaenda kuweka historia nyingine ambayo iliwekwa miaka 30 iliyopita na Gidamis Shahanga,” amesema Akhwari.

RIAD 02

Derek Froude ni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Posso Sports ambayo inamsimamia nyota huyo, amesema mwaka 2025 umekuwa wa mafanikio kwa Tanzania katika mchezo wa riadha kwani nyota wake wamefanya kweli na kuitangaza vyema kimataifa, akiwemo Alphonce Simbu ambaye alishinda medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia, Magdalena Shauri aliyemaliza nafasi ya tatu, Chicago Marathon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *