
Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amejigamba kuwa jeshi lake lilishambulia Ukanda wa Ghaza siku ya Jumapili kwa tani 153 za mabomu, ambayo ni sawa na kukiri kwamba utawala huo ghasibu umekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano uliyofikia na harakati ya Hamas kupitia mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani.
Akihutubia ufunguzi wa kikao cha bunge la utawala wa kizayuni, Knesset, Netanyahu alikatishwa hotuba yake mara kwa mara na wabunge wa upinzani wanaopinga sera za serikali yake na hatua yake ya kurefusha kwa makusudi vita vya Israel huko Ghaza.
“Wakati wa usitishaji mapigano, wanajeshi wawili walikufa… Tuliwapiga kwa tani 153 za mabomu na kushambulia makumi ya shabaha katika Ukanda wa Ghaza,” alieleza Netanyahu kwa majigambo.
Ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imeripoti ukiukaji 80 wa usitishaji mapigano ambao umefanywa na Israel tangu makubaliano hayo yaliyofadhiliwa na Marekani yalipoanza kutekelezwa tarehe 10 Oktoba, na kupelekea kuuawa shahidi Wapalestina wapatao 100, wakiwemo 44 waliouawa siku ya Jumapili pekee, na wengine 230 kujeruhiwa.
Tel Aviv ilidai kuwa Hamas ilishambulia vikosi vyake katika mji wa kusini wa Rafah. Hata hivyo harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina imekanusha kuhusika kwa namna yoyote na shambulio hilo na kusisitiza kuwa imejifunga kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano.
Makubaliano ya kusitisha vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Ghaza yalitangazwa Oktoba 10, kwa kuzingatia mpango wa awamu uliowasilishwa na Rais wa Marekani Donald Trump. Awamu ya kwanza ilijumuisha kuachiliwa kwa mateka wa Israel mkabala wa wafungwa wa Kipalestina.
Mpango huo pia unatazamia kujengwa upya kwa Ghaza na kuanzishwa mfumo mpya wa utawala utakaoitenga harakati ya Hamas.
Wa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ghaza tangu Oktoba 2023 hadi sasa, vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel yameshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 68,200 na kujeruhi zaidi ya 170,200…/