
Uchambuzi wa Qur’ani kuhusu tabia ya Donald Trump, rais mtata wa Marekani, unamuonyesha kuwa ni mfano wa wazi wa mtu muovu na mwenye kutakabari.
Katika Quran, uistikbari na kutakabari kunamaanisha kupenda makuu, kiburi, kujiona kuwa muhimu, kukataa kukubali haki na ukweli, na uasi dhidi ya sheria na akili timamu. Sifa hizi zinaweza kuvuka kiwango cha mtu binafsi na kuwa jambo la kijamii lenye matokeo mabaya kwa jamii.
Katika Qur’ani tukufu, neno ustikabri na minyambuliko yake limekaririwa mara 48. Fasili na maana hizi zote zinasisitiza kulaani vikali tabia ya kiburi na kiistikbari na kuitambulisha kuwa tabia mbaya na isiyofaa.
Quran inaorodhesha mambo kadhaa katika kuundika na kujitokeza tabia hii ya kujiona na kupenda makuu na dharua kupita kiasi dhidi ya wengine. Baadhi ya mambo hayo ni mali, nguvu za kijeshi na kisiasa, umaskini wa kiutamaduni, udanganyifu wa ubora katika uumbaji, ukafiri, kufuata matamanio ya mtu mwenyewe, dhambi, na kupuuza uwezo wa kiungu. Sababu hizi zinaweza kusababisha tabia ya kiburi kwa watu binafsi na jamii.
Kwa mtazamo wa Qur’ani, kiburi, uistikabri na kujiona ni jambo ambalo lina matokeo ya uharibifu ambayo yanajidhihirisha katika ngazi ya mtu binafsi na ya kijamii.
Baadhi ya matokeo haya ni pamoja na:
- Kuvunja ahadi: Watu wenye kiburi, kwa sababu ya kujiona kuwa muhimu, hawafungamani ahadi zao na hawako tayari kuwatendea usawa watu wengine.
- Shutuma na uwongo: Wanajiona kuwa wao pekee yao ndio walio katika haki na kuwaita wengine waongo.
3. Kuwaangamiza wa wapinzani: Watu wenye kiburi hukabiliana kwa ukali na upinzani wowote kwa tamaa zao, hata kufikia hatua ya kuwaondoa wapinzani kimwili au kishakhsia.
4. Kupinga haki: Wanachukulia ishara au sauti yoyote ya haki na ukweli kuwa ya uwongo na batili na hivyo wanaipinga.
5 . Matakwa yanayokinzana na akili: Kwa sababu watu wenye kutakabari hujiona kuwa wao ni bora zaidi, hutoa matakwa ambayo hayana mantiki na haki kutoka kwa wengine.
6. Ukaidi na kutoikubali haki: Kwa sababu watu wa aina hii hujuina na kujikweza huwa hawako tayari kuikubaki haki na hivyo husimama kuipinga na kukabiliana nayo.
7 . Hisia za kiburi na mamlaka: Wanajiona kuwa bora kuliko wengine na kuwaona wengine kuwa hawana akili na ustahiki.
8 . Udhalimu na ubabe: Hatimaye, mtazamo huu hupelekea kuibuka tabia ya kidikteta na kulazimisha maoni kwa wengine.
Marekani ni nembo ya ubeberu na mabeberu
Ubeberu na uistikbari wa kisiasa unaelezwa katika Quran kuwa ni utawala usio wa haki na satwa dhidi ya wengine. Waistikbari na mabeberu wa kisiasa ni wale wanaonyakua madaraka kinyume cha sheria, wanawaona watu kuwa ni wadogo na wajinga, na wanajiona kuwa ni walinzi na wakubwa wao.
Aina hii ya ubeberu ni kinyume na misingi ya kifitra na kimaumbile, kimantiki na kidini, na katika kipindi chote cha histori, watu kama vile Firauni na Namrudi walikuwa alama na nembo za hilo. Qur’ani tukufu sambamba na kuashiria tabia ya Firauni, inamtambulisha kuwa ni fisadi aliyegawanya watu makundi makundi, akawadhoofisha baadhi, akawaua watoto wao, na kuwafanya watumwa wanawake wao.
Kwa ujumla, Quran, kwa kuchambua kwa makini sifa za wenye kiburi, inatoa picha ya shakhsia inayowiana na tabia ya Donald Trump. Kwa mtazamo wa Qur’ani, mtu kama huyu anaweza kuwa chanzo cha ufisadi, uonevu, na dhulma sio tu kwa kiwango cha mtu binafsi bali pia katika ngazi ya kimataifa.
Katika enzi ya sasa, Marekani inajulikana kama alama na nembo ya ubeberu na uistikabari wa kimataifa kutokana na misimamo yake ya upande mmoja na kujiona kuwa yenyewe tu ndio iliyo katika haki. Sifa hizi zimedhihirika hasa katika tabia ya Donald Trump, rais mtata wa Marekani.
Shakhsia na utendaji wa Trump yanawiana na sifa za watu waistikbari na wenye katika Quran. Yeye ni mfano wa wazi wa mtu mwenye ubeberu wa kisiasa, kwa kuvunja kwake ahadi, kashfa, kuwaangamiza wapinzani, kupinga haki, kutoa matakwa yasiyo ya kimantiki, ukaidi, kiburi, tamaa ya mamlaka, na dhulma.
Trump sio tu amekuwa na tabia ya dharau na kejeli kwa wakuu wa nchi zingine katika uga wa kimataifa, lakini pia amejionyesha kuwa mfalme mutlaki ndani ya Marekani. Mfano wa tabia hii ulikuwa ni mkutano wa kilele wa Sharm el-Sheikh huko Misri, ambapo Trump alionyesha kejeli na dharau kubwa kwa wakuu wa mataifa mengine hususan Rais wa Misri aliyekuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Nchini Marekani, tabia yake ya kibeberu imepelekea kuibuka maandamano yaliyoenea nchi nzima chini ya kaulimbiu “Hapana kwa Mfalme.” Katika radiamali yake kwa maandamano hayo, aliyakejeli kwa kusambaza video ya Akili Mnemba ambapo alionekana akiwa ndani ya ndege ya kijeshi akiwadondoshea matope waandamanaji kutoka angani, hatua ambayo inaonyesha kuporomoka kwa maadili.
Njia za kukabiliana
Katika kukabiliana na shakhsia kama hii ya kibeberu, Qur’ani haipendekezi kuamiliana naye kwa ulaini na upole. Badala yake, inasisitiza kwamba kushughulika na watu wenye kiburi kunapaswa kufanyika kwa nguvu, uimara na ukosoaji.
Sera za Trump za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja, ikiwa ni pamoja na vita vya kibiashara na madai ya umiliki wa nchi kama Kanada na Greenland, bila shaka zitachukua wigo mpana siku baada ya siku endapo hakutakuweko na upinzani wa kimataifa.
Njia ya kukabiliana na utendaji huu ni kutegemea uwezo wa ndani wa nchi, kuhifadhi heshima ya kitaifa, na kuchukua misimamo iliyo wazi na muhimu dhidi ya mienendo na tabia za satwa.
Trump ameonyesha mara kwa mara kwamba, anaelewa tu lugha ya mabavu, na kila aina yoyote ya ulaini na kuonyesha udhaifu mbele yake, hakutakuwa na natija yoyote ghairi ya kumuongezea kiburi na ujeuri. Kwa muktadha huo, ili kukabiliana na ubeberu wa kisiasa kunahitajika kusimama kidete na welewa na wakati huo huo mataifa na serikali kupigania heshima yao na kutokubali kunyongeshwa.