Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, ameanza kutumikia kifungu cha miaka mitano jela katika gereza moja mjini Paris baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ufisadi.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 70 aliwasili katika gereza la La Sante kwa gari la polisi mapema leo Jumanne na kuwa mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi ya Umoja wa Ulaya kufungwa jela.

Mwezi uliopita, Sarkozy alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya njama ya uhalifu, kutokana na kupokea mamilioni ya euro kama malipo haramu kutoka kwa mtawala wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, ili kufadhili kampeni yake ya uchaguzi wa rais 2007.

Sarkozy amekuwa akikana tuhuma hizo. Mawakili wake wamesema alipofika gerezani kwa ajili ya kuanza kifungo chake kwamba wamewasilisha ombi la kuachiliwa huru mara moja.

Sarkozy anakuwa kiongozi wa kwanza wa Ufaransa kufungwa jela tangu Philippe Petain, aliyekuwa kiongozi wa serikali mshirika wa Manazi, ambaye alifungwa jela baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Kuna uwezekano kwamba Sarkozy atazuiliwa katika seli iliyojitenga, ambapo wafungwa huwekwa katika kifungo cha upweke na kufanya shughuli nje ya seli kwa kutenganishwa kwa sababu za kiusalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *