
Waandishi wa Shirika la Habari la Ufaransa, AFP wamemuona Sarkozy mwenye umri wa miaka 70 akiondoka nyumbani kwake asubuhi ya leo na baada ya muda mfupi akaingia katika gereza la La Sante lililoko mjini Paris, akisindikizwa na maafisa wa polisi.
Sakorzy atatumikia kifungo cha miaka mitano jela. Mawakili wake wamesema wamewasilisha ombi la kutaka kuachiwa kwake.
Sarkozy aliyeiongoza Ufaransa kutoka mwaka 2007 hadi 2012, mwezi uliopita alipatikana na hatia ya kutafuta ufadhili wa kampeni kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya Muamar Gadafi, katika uchaguzi ambao alishinda.
Wafuasi wake kadhaa walikuwa nje ya makaazi yake mapema leo, huku baadhi yao wakiwa wamebeba mabango yenye picha zake.
Sarkozy sasa ndiye kiongozi wa kwanza wa Ufaransa kufungwa jela tangu Rais Philippe Petain, ambaye alishirikiana na utawala wa Kinazi. Petain alifungwa jela baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.