Hukumu dhidi ya Sarkozy inachukuliwa kama anguko kubwa kwa kiongozi huyo aliyeiongoza Ufaransa kati ya mwaka 2007 hadi 2012.

Rais huyo wa zamani aliondoka nyumbani kwake mapema Jumanne akiwa na mkewe Carla Bruni huku akishangiliwa na umati wa wafuasi wake waliokuwa pia wakiimba wimbo wa taifa wa Ufaransa.

Sarkozy aliyehukumiwa kifungo hicho mwezi uliopita atakuwa rais wa kwanza wa zamani wa Ufaransa kuhukumiwa kifungo tangu Rais Marshal Philippe aliyehukumiwa kifungo baada ya Vita vya Pili vya Dunia kutokana na kushirikiana na wanajeshi wa Kinazi.

Sarkozy, “Sina hatia”

Muda mfupi baada ya kuingia kwenye gari kuelekea kwenye gereza hilo la La Sante, Sarkozy alichapisha ujumbe mrefu kwenye mtandao wa kijamii wa X uliolezea alikuwa muhanga wa chuki na kisasi. “Ninataka kuwaambia watu wa Ufaransa, kwamba si rais wa zamani wa Jamhuri ambaye anafungwa leo asubuhi – ni mtu asiye na hatia.”

Ufaransa Paris 2025 | Rais wa zamani Nicolas Sarkozy akimkumbatia mkewe Carla Bruni kabla ya kwenda gerezani
Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akimkumbatia mke wake Carla Bruni-Sarkozy wakati akiondoka kwenye makazi yake kwenda kwenye Gereza la La Sante baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.Picha: Julien De Rosa/AFP/Getty Images

Hukumu ya Sarkozy inahitimisha miaka kadhaa ya mivutano ya kisheria kufuatia madai kwamba alipata ufadhili wa mamilioni ya fedha za kampeni zake za urais za mwaka 2007 kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, ambaye baadae alipinduliwa na kuuawa wakati ya vuguvugu la maandamano yaliyoshuhudiwa katika nchi za Kiarabu na kusababisha mapinduzi. 

Hata hivyo, Sarkozy amekana madai hayo na ameiita kesi hiyo kuwa iliyochochewa kisiasa, huku wakili wake Christophe Ingrain akiwaambia waandishi wa habari kwamba wamewasilisha ombi la kuachiliwa kwa mteja wake muda mfupi tu baada ya kufika gerezani.

Wafuasi washuhudia akienda gerezani

Baadhi ya wafuasi wake waliokusanyika kwenye makazi yake yaliyoko kwenye mtaa wa kitajiri mjini Paris mapema leo kushuhudia kiongozi wao akiondoka kwenda gerezani walionyesha kutoridhishwa kabisa na madhila dhidi yake, baada ya mwanae wa kiume Louis mapema Jumanne hii kuwaomba kuonyesha kumuunga mkono baba yake.

Ufaransa Paris 2025 | Nicolas Sarkozy na Carla Bruni-Sarkozy wakiondoka nyumbani kwao kuelekea gerezani
Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akiwapungia wafuasi wake wakati alipokuwa akiondoka nyumbani kwao mjini Paris kuelekea jela kuanza kutumikia kifungo cha miaka mitano.Picha: Thibault Camus/AP Photo/dpa/picture alliance

Mmoja ya wafusi hawa ni Michelle Perié, mama mwenye umri wa miaka 67, alisema “Niko hapa kwa sababu ya ghadhabu na dhuluma. Hatuelewi… hatuelewi. Rais wa zamani… hatuelewi. Kwanza, hatendewi haki kama wengine. Ni mtu anayejua siri za serikali. Ni mtu ambaye amekuwa akiifanya kazi yake, alisimama imara.. hatuelewi.”

Muda mfupi kabla ya kuingia gerezani, Sarkozy na mkewe walionekana wakitembea taratibu kwenda kuungana na watoto wao Jean, Pierre, Louis na Giulia pamoja na wajukuu zao ambao pia walikuwa nje ya nyumba, kisha kuupungia mkono umati wa wafuasi wake kisha akaingia kwenye gari lake.

Bado anapinga hukumu na uamuzi anaosema sio wa kawaida wa jaji kumtia ndani akisubiri rufaa na safari yake kutoka Ikulu ya Elysée hadi kwenye gereza la La Santé imeibua maswali kwa Wafaransa wengi.

Kulingana na mawakili wake, Sarkozy atazuiwa kwenye chumba cha peke yake  na kutengwa na wafungwa wenzake kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, wamesema tayari alikwishajiandaa kisaikolojia na kimwili. Aliandaa nguo kama masweta kwa kuwa vyumba hivyo huwa na baridi kali na kelele nyingi. Wamesema ni wazi atapitia mateso makali, lakini amejiandaa.

Na yeye mwenyewe Sarkozy aliliambia gazeti la La Tribune Demanche kwamba haogopi jela, atakuwa jasiri hata atakapofika mbele ya milango ya gereza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *