SIMBA ni kama imetanguliza mguu mmoja ndani ya kundi mojawapo la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, baada ya kuichapa Nsingizini Hotspurs ya Eswatini kwa mabao 3-0 kule kwao Mbabane, na wiki hii inamalizana na wapinzani wao kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kutokana na hilo, kuna tambo nyingi zinaendelea katika mtaa wa Msimbazi yalipo maskani ya Simba, lakini nyuma ya hilo mtendaji mkuu wa zamani wa Simba na Yanga, Msauzi Senzo Mazingiza amefichua siri za nyota wapya wa Wekundu wa Msimbazi.

Senzo amewazungumzia wachezaji wa zamani wa mabingwa wa Afrika Kusini, Neo Maema na Rushine de Reuck waliotua kikosini Msimbazi msimu huu.

Mtendaji huyo wa zamani aliyeanza kuiongoza Simba mwaka 2019 kabla ya kutua Yanga 2021, amesema nyota hao waliamua kuchagua kucheza Tanzania kutokana na ukubwa wa klabu hiyo na uwepo wa aliyekuwa kocha Fadlu Davids ambaye baadaye alihamia Raja Casablanca ya Morocco, huku akianika bayana uwezekano wa wachezaji zaidi wa Afrika Kusini kujiunga na Ligi ya Tanzania siku za usoni.

SENZ 01

Maema na De Reuck walijiunga na Simba baada ya kuondoka Mamelodi Sundowns na awali wachezaji hao walihusishwa na klabu kadhaa za Sauzi, lakini hatimaye wakasaini kwa klabu hiyo yenye maskani yake makuu Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Senzo, kwanza wachezaji hao wakati wanasaini, Fadlu Davids alikuwa kocha wa Simba, ingawa sasa amehamia kwa miamba wa Morocco, Raja Casablanca. 

Pili, Simba ilikuwa na tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo lililowavutia sana, licha ya kukiri watakabiliwa na changamoto za hasira za mashabiki wasio na uvumilivu pale wakizembea kidogo.

Mbali na Simba, klabu nyingine kubwa kwa Tanzania ni Yanga na Azam FC na kwa mujibu wa Senzo ni kwamba klabu hizo zina uwezo wa kushindana na timu za Afrika Kusini katika suala la mishahara.

Akizungumza na Chama cha Waandishi wa Habari za Soka Afrika Kusini (SAFJA), Senzo ambaye kwa mara ya kwanza alitua Simba Septemba 2019 akitangazwa kuwa CEO, amesema: “Tanzania kuna klabu nne au tano ambazo zinalipa vizuri. Ninaposema vizuri namaanisha mishahara inayoweza kumshawishi mchezaji kuondoka kwao na kuhamia Tanzania, kitu kilichowafanya hata kina Maema na De Reuck kusajiliwa Simba.

SENZ 02

“Utakuta wachezaji wengi katika klabu hizo nne ni wageni. Kwa mfano Yanga wana wachezaji takriban 10 hadi 12 kutoka nje ya nchi. Malipo ni mazuri kwa kweli, lakini ukiweka timu ya Afrika Kusini na ya Tanzania zikishindania mchezaji, timu ya Afrika Kusini mara nyingi ingeshinda dili. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kuwa timu za Tanzania haziwezi kulinganisha mishahara, wanaweza, na hata posho za usajili pamoja na mazingira ya maisha ni mazuri.”

Senzo ambaye alikuwa CEO wa Yanga kwa kipindi cha msimu mmoja wa 2021-2022 alipotua baada ya kuondoka Simba, ameongeza kwamba: “Tanzania imekuwa nzuri na inaendelea kuwa bora. Dar es Salaam ni jiji zuri kuishi, ni la kisasa. Changamoto pekee kwa wachezaji wageni ni lugha, lakini hilo linaweza kuzoeleka kwa muda. 

PANT 01

“Sidhani kama wachezaji kutoka Afrika Kusini watapata ugumu mkubwa kuishi Tanzania. Hata hivyo, kuna changamoto zake. Tanzania inaweza kuwa mahali pazuri sana kwako, lakini mambo yakibadilika, unaweza kuhisi hasira za mashabiki. Ni jambo zuri kuona wachezaji wakifikiria soko hilo, ingawa sina uhakika kama wengi watataka kwenda huko.”

De Reuck ambaye ni beki wa kati, mapema tu imeonekana amejihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza akiwa amecheza mechi zote sita za mashindano, akifunga mabao mawili ndani ya Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wa Maema anayemudu nafasi ya kiungo mshambuliaji, bado anajitafuta japo ujio wa kocha Dimitar Pantev umemfanya aanze kikosi cha kwanza katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Nsingizini Hotpsurs ambapo Mnyama alishinda mabao 3-0.

PANT 02

Kila msimu, Simba imekuwa ikitenga bajeti inayopanda kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya klabu hiyo ikiwemo usajili. Msimu uliopita 2024-2025, Simba ilitangaza bajeti ya Sh28.6 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh3 bilioni kutoka bajeti ya 2023-2024 iliyokuwa Sh25 bilioni.

Kwa upande wa Yanga, bajeti yao ya msimu huu 2025-2026 imetangaza itatumia kiasi cha Sh33 bilioni ikiwa ni ongezeko la takribani Sh8 bilioni kulinganisha na iliyopita 2024-2025 ambayo ni Sh25.3 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *