
Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimeripotiwa kushambulia maeneo muhimu katika mji mkuu wa Sudan, ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo.
Gazeti la Rakoba la Sudan, likinukuu mashuhuda, limeripoti leo Jumanne habari ya kujiri miripuko minane ndani na karibu na uwanja huo wa ndege.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya nchi hiyo ilisema jana Jumatatu kwamba, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum utaanza tena safari za ndani kuanzia Jumatano hii, baada ya kufungwa kwa miezi 30 kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo.
Ripoti ya vyombo vya habari nchini humo ilielezea shambulio hilo kama “jaribio la wazi la kutatiza kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege baada ya kufungwa kwa zaidi ya miaka miwili.”
Ripoti kutoka angatua hiyo zilionyesha kuwa, jeshi la Sudan limefanikiwa kutungua ndege kadhaa zisizo na rubani, huku zingine zikishambulia shabaha zao, na kusababisha hofu katika vitongoji vya karibu, chombo hicho kiliongeza.
Mwezi Machi, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limedhibiti Uwanja wa Ndege wa Khartoum, pamoja na vituo kadhaa vya usalama na kijeshi na vitongoji kadhaa mashariki na kusini mwa mji mkuu kwa mara ya kwanza tangu vita vilipozuka.
Jeshi la Sudan na waasi wa RSF wamekuwa wakipigana tangu mwezi Aprili mwaka 2023; vita ambavyo hadi sasa vimeuwa watu zaidi ya 20,000 na kusababisha wengine milioni 14 kuwa wakimbizi.