UNAJUA nini? Lazima Silver Strikers wafe kwa Mkapa. Hiyo ndiyo kauli inayombea mitaa ya Twiga na Jangwani yalipo maskani ya Yanga ambapo mashabiki wameungana na uongozi kuhakikisha kwamba wanalipiza kisasi kwa kuifumua timu hiyo kutoka Malawi ili wafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga imeingia kazini kuanza hesabu za kupindua meza dhidi ya Silver Strikers, huku mashabiki katika eneo la mzunguko kasoro VIP A na B, lakini kwingine kote ni bure.

Lakini kabla ya mechi hiyo inayopigwa Jumamosi, wiki hii majira ya saa 11:00 jioni kuna vikao vitatu vizito vitafanyika kabla ya kwenda kumalizana na Wamalawi hao.

Iko hivi; Yanga inaingia kwenye kipindi ambacho wamekipa jina la Wiki ya Heshima ikitaka kuhakikisha inakinusuru kikosi na aibu ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

YANG 04

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, amefichua kwamba haitakuwa rahisi kwao kukubali kutolewa na Wamalawi hao na uongozi wao utatinga kambini kuanzia leo kwanza kuzungumza na kocha wa muda, Patrick Mabedi kuangalia kipi anahitaji ili wapindue meza.

Yanga baada ya kurejea nchini juzi Jumatatu, jana Jumanne mchana kikosi kikaingia kambini kuanza maandalizi ya mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.

Yanga itahitaji ushindi wa tofauti ya mabao angalau 2-0 ili kuikomboa tiketi ya kwenda makundi kwa msimu wa nne mfululizo kwenye mashindano ya CAF.

YANG 03

Gumbo alisema mbali na kikao na Mabedi ambaye ni raia wa Malawi, watakutana pia na wachezaji wao kuwaongezea morali kwenye maandalizi yao na hata mechi hiyo.

Bosi huyo aliongeza kuwa, wana imani kubwa kwamba licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi kufuatia kumfuta kazi aliyekuwa kocha mkuu, Romain Folz, lakini wana kikosi imara ambacho kinaweza kubadili matokeo hayo.

“Huu ni mchezo muhimu dhidi ya Silver Strikers, nataka kukwambia maandalizi ya mchezo huu sio ya kawaida, ni kama tunakwenda kucheza fainali, unaona ambavyo tumewahi kuingia kambini, timu inaingia kambini leo (jana) hatuna muda wa kupoteza,” amesema Gumbo.

“Uongozi wetu utakwenda kambini wakati wowote kuanzia kesho (leo) tutatangulia kukutana na kocha atatueleza kama kuna kitu anahitaji ili akipate kwa haraka na baada ya hapo tutakutana na wachezaji wa timu nzima, tunataka kuhakikisha saikokolojia yao inakuwa ni kuhusu kushinda kikubwa.

YANG 02

“Kupitia chombo chako wafikishieni salamu mashabiki wetu kwamba tupo timamu na wao wajipange, hii ni mechi yetu waje uwanjani lakini tuna jukumu la kushirikiana kurudisha heshima yetu, haitakubalika tushindwe kufuzu mara mbili mfululizo hatua ya makundi.”

Wakati Gumbo akiyasema hayo, taarifa zaidi kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, mabosi hao watakuwa na kikao cha tatu kizito juu ya kupata muafaka wa nani atakuwa kocha wao mpya badaa ya kuachana na Folz.

YANG 01

Yanga inajipanga kuhakikisha ndani ya wiki moja wanapata muafaka nani atakuja kuwa kocha wao ambaye wanaweza kumtangaza mapema wiki ijayo baada ya kumaliza mchezo dhidi ya Silver Strikers.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *