Mbeya. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa mwongozo kwa wananchi waliopoteza kitambulisho cha mpigakura kutumia leseni za udereva, kadi ya Nida na pasi za kusafirisha huku wasioona wakitumia mfumo wa nukta nundu.

Hatua hiyo imetajwa kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika kupigakura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano Oktoba 29, 2025.

Msimamizi wa uchaguzi majimbo ya Mbeya Mjini na Uyole, Anamary Mbunga ametoa mwongozo huo wa INEC, leo Jumanne Oktoba 21, 2025, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, zikiwa zimebaki siku nane kabla ya uchaguzi.

“Ni lazima kila mpigakura afike kwenye kituo cha kupigia kura akiwa na kadi yake, lakini kwa wale walipoteza wafike mapema kwenye vituo walikoboresha taarifa zao kwenye daftari la mpigakura sambamba na leseni ya udereva, Nida au pasi ya kusafiria ambavyo vina majina sahihi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mbunga amesema kwa majimbo ya Mbeya Mjini na Uyole, kuna vituo 900 vya kupigia kura, lakini kwa Mbeya Mjini kuna kata 23 badala ya 36 za awali kabla hayajagawanywa.

Wakati huo huo amesema kwa sasa wagombea wote wa vyama vinavyo shiriki uchaguzi wanaendelea kufanya kampeni na wananchi  wanajitokezq kusikiliza  sera za vyama vyote.

“Niwahakikishie wananchi kama jinsi kampeni zinavyoendelea kwa usalama ndivyo siku ya uchaguzi kutakuwa salama, kikubwa niwahamasishe kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025,” amesema.

Ametaja vyama 12 vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu katika majimbo hayo ni pamoja na ACT-Wazalendo, CCM, DP, Chaumma, CUF, NLD, NRA, Ada-Tadea, TLP, AAFP, Demokrasia Makini na CCK.

Kuhusu kundi la wazee na walemavu, amesema kuna utaratibu utawekwa kuchagua watu watakaowaongoza kwenye chumba cha kupigia kura ikiwepo kundi la wenye ulemavu  wasioona, watatumia mfumo wa nukta nundu.

Hali ya maandalizi

Mbunga amesema maandalizi ya uchaguzi katika majimbo hayo yamekamilika na kuwataka wananchi kujitokeza kutimiza takwa la msingi sambamba na kuhakikisha kuwepo kwa hali ya usalama katika vituo vyote vya kupigia kura.

“Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni lakini kwenye maeneo ya Magereza wataanza saa 1:00 asubuhi hadi saa 9:00 jioni” amesema.

Akizungumzia uchaguzi huo, mfanyabiashara wa bidhaa za majumbani, Peter Fredy alisema ni lazima ajitokeze kupiga kura na kutimiza haki yake ya msingi na kuhamasisha vijana wenzake.

“Wakati wa vurugu za uvunjifu wa amani ulipita, kimsingi tunaomba Serikali kuhimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya makazi ya watu, shuli za kiuchumi na vituo vya kupigia kura, lakini pia, kuboresha miundombinu ya watu wenye ulemavu,” ameongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *