WFP hata hivyo imeeleza kwamba kiwango cha usambazaji bado kiko chini ya lengo lake la kila siku la tani 2,000 kwa sababu vituo viwili pekee vya mipakani ndivyo vilivyofunguliwa hadi sasa. 

Kulingana na WFP, takriban tani 750 za chakula zinaingia katika Ukanda wa Gaza kila siku, lakini kiwango hicho bado kiko chini sana ya mahitaji baada ya miaka miwili ya vita kati ya Israel na kundi la Hamas, vita ambavyo vimeharibu sehemu kubwa ya Gaza na kuifanya idadi kubwa ya wakaazi wake kusalia bila makaazi rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, msemaji wa shirika hilo Abeer Etefa amesema wanapaswa kutumia kila kituo cha mpakani ili kuongeza usambazaji zaidi wa chakula ndani ya Gaza.

Etefa ameongeza kwamba, ni vituo viwili pekee vinavyodhibitiwa na Israel ndivyo vinavyofanya kazi ambavyo ni vya Kerem Shalom upande wa Kusini na Kissufim, katikati ya Gaza.

“Tangu kusitishwa kwa mapigano tarehe 11 Oktoba, sasa tuna zaidi ya malori 100 na zaidi ya malori 530 yameingia Gaza ili kusaidia usambazaji wa mikate, programu za lishe, na usambazaji wa chakula kwa ujumla. Hadi sasa, tumekuwa na zaidi ya tani 6,700 za chakula. Kiasi hicho kinatosha kukidhi mahitaji ya karibu watu nusu milioni kwa muda wa wiki mbili. Usambazaji unaendelea kila siku, na sasa tunapata wastani wa tani 750.” 

Lengo la WFP ni kuingiza tani 2,000 za chakula kila siku Gaza

Msemaji huyo wa WFP ameeleza kwamba baadhi ya misaada ya lishe kwa watoto na wanawake wajawazito imefika upande wa kaskazini mwa Gaza, lakini misaada hiyo bado iko chini ya kiwango kinachohitajika.

Wakaazi wengi wa Gaza wanahifadhi chakula wanachopokea kutokana na wasiwasi kwamba zoezi la usambaji wa chakula linaweza kuzuiwa tena.

Kulingana na Etefa, misaada iliyotolewa hadi sasa ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya takriban watu nusu milioni katika muda wa takriban wiki mbili.

“Kiwango cha tani 750 ni kikubwa tofauti na tulichokuwa nacho kabla ya kusitishwa kwa mapigano, lakini hata hivyo bado kiko chini ya lengo letu, ambalo ni karibu tani 2,000 kila siku,” ameongeza Etefa.

Palestina | Gaza | Usambazaji wa chakula | WFP
Wapalestina wakipigania chakula katika eneo la usambazaji wa chakula. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linasema karibu mtu mmoja kati ya watatu katika ukanda wao Gaza anakosa chakula kwa siku kadhaa Picha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amewasili nchini Israel na anatarajiwa kufanya mazungumzo katika wakati ambapo Washington inajaribu kunusuru awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.

Vance anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na viongozi wengine waandamizi wa serikali, na inaripotiwa kwamba huenda akasalia huko hadi siku ya Alhamisi.

Ziara yake inafuatia ile iliyofanywa jana Jumatatu na mjumbe maalum wa Donald Trump katika eneo la Mashariki ya Kati Steve Witkoff na Jared Kushner, mkwe wa Rais Trump.

Makamu huyo wa Rais wa Marekani pia amepangiwa kukutana na familia za mateka ambao miili yao bado inazuiliwa ndani ya Gaza na baadhi ya mateka walioachiliwa wiki iliyopita chini ya makubaliano ya usitishaji mapigano.

Mapema leo, Witkoff na Kushner walikutana na mateka tisa kati ya mateka walioachiliwa huru.

Ziara ya Vance nchini Israel ameifanya baada ya Israel na Hamas kutupiana lawama mara kadhaa kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano tangu yalipotiwa saini rasmi siku nane zilizopita, huku kukishuhudiwa vurugu za hapa na pale na kujikokota kwa kasi ya kuirejesha miili ya mateka wa Israel, hali ambayo inaibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa makubaliano hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *