Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imelaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya Mtanzania vinavyoonekana kupitia picha jongevu na video zinazozagaa mitandaoni, zikionesha baadhi ya watu wakicheza ngoma na muziki usio na staha katika maeneo ya wazi, vyombo vya usafiri na makazi binafsi.
Katika taarifa yake kwa umma, Wizara imesisitiza kuwa vitendo hivyo vinakiuka misingi ya maadili ya Mtanzania na vinaweza kusababisha taharuki na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Aidha, Wizara imeagiza wadau wote wanaopata taarifa za matukio ya aina hiyo kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka husika ikiwemo Wizara yenyewe, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika kama ilivyokuwa kwa wengine waliowahi kukutwa na makosa kama hayo.
Wizara pia imeonya wananchi dhidi ya kuendelea kusambaza picha au video hizo mtandaoni, ikieleza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, inayokataza usambazaji wa maudhui yasiyo na maadili. Imesisitiza kuwa usambazaji wa maudhui hayo unaongeza madhara kwa jamii na ni kosa la kisheria.
✍ Mwandishi Wetu
Mhariri @claud_jm
#AzamTVUpdates