NYOTA wa zamani wa Taifa Stars, Yanga na Simba, Willy Martin, amesema amefuatilia vyema mechi za wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ngazi ya klabu msimu huu na kubaini timu hizo zinaweza kufuzu makundi.

Pamoja na matumaini hayo, nyota huyo ametoa angalizo kwa Yanga kutowadharau wapinzani wao na kucheza kwa mazoea, akieleza kuwa wanapaswa kukaza ili kuendeleza heshima kimataifa.

Tanzania ina wawakilishi wanne, ikiwa Azam na Singida Black Stars zinashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, huku Yanga na Simba zikikipiga Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hizo zilianzia ugenini katika mechi za kwanza hatua ya pili, ambapo Simba ilishinda 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs nchini Eswatini, timu hizo zinarudiana Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

YANG 01

Kwa upande wa Yanga, ililala bao 1-0 mbele ya Silver Strikers nchini Malawi, zinarudiana Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM huko visiwani Zanzibar, marudiano ni Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, ilhali Singida Black Stars ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Flambeau du Centre nchini Burundi, nazo zinarudiana Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Akizungumza na Mwanaspoti, Martin amesema anayo matumaini makubwa kwa timu zote hizo kufuzu hatua ya makundi, lakini Yanga inapaswa kuacha mazoea na badala yake kuheshimu wapinzani.

YANG 02

Amesema rekodi iliyowekwa hadi sasa kwa timu hizo, itakuwa fahari kubwa kuona Tanzania inaingiza wawakilishi wake kwenye hatua inayofuata akiwapa pongezi wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hizo.

“Timu zote zinaweza kufuzu, niwaombe Yanga wasiwadharau wapinzani wakacheza kwa mazoea kwamba wao ni wakubwa, mpira hauko hivyo, kipekee niwapongeze wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu zote,” amesema Martin.

Mkongwe huyo ameongeza kuwa, pamoja na matokeo ya timu zote, lakini kila mmoja anapaswa kujipanga kwakuwa mpira hauna cha nyumbani wala ugenini, akiwaomba mashabiki na wadau wa soka nchini kutoa sapoti.

YANG 03

Amesema kwa sasa soka la Tanzania linafuatiliwa kutokana na ubora na ushindani wa timu, hivyo kufuzu makundi kwa timu nne utaongeza heshima na thamani kwa Taifa nje ya mipaka.

“Kila mmoja ajipange kusaka matokeo mazuri, tuna bahati wote watakuwa nyumbani, mashabiki na wadau watoe sapoti kubwa ili Tanzania izidi kung’ara kimataifa kwakuwa heshima tunayo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *