
Akizungumza katika kongamano hilo la kitaaluma na uzinduzi wa hifadhi ya kidijitali ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Waziri wa Elimu wa Zanzibar Lela Mohamed Mussa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kwa niaba ya Rais Hussein Mwinyi amemuelezea Mzee Karume kuwa ni mzalendo na mwanamapinduzi wa kweli.
Kigoda cha Mzee Karume kipo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Makamu Mkuu wa SUZA, Profesa Mohammed Makame, ametumia mkusanyiko huo kuelezea nafasi na harakati za ukombozi Afrika.
Amesema SUZA imechukua hatua ya historia ya kuhifadhi kidijitali na hazina ya kitaifa inayokusanya nyaraka picha, kumbukumbu za Mzee Karume kwa lengo la kuhifadhi na kufanyiwa tafiti.
Mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo ni pamoja na nini cha kujifunza kutoka uongozi wa Mzee Karume; na amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mada ambayo iliwasilishwa na Profesa Patrick Lumumba kutoka Kenya ambapo alisisitiza viongozi kuwa na miiko na maadili.
Kongamano hilo lilihitimishwa kwa kaulimbiu ”Maisha ya Sheikh Abeid Amani Karume na Urithi kwa Vijana: Amani, Mshikamano na Demokrasia kuelekea uchaguzi mkuu 2025”, likiwa ni sehemu ya juhudi za kudumisha fikra, falsafa na urithi wa hayati Karume kwa vizazi vijavyo.
Kigoda cha Mzee Karume majukumu yake yanafanana na kidoga cha Mwalimu Nyerere cha Tanzania Bara, ambapo jukumu lake ni kujikita katika masuala ya kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya maendeleo nchini. Salma Said, DW, Zanzibar.