
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Watu 46 wamepoteza maisha na wengine wamejeruhiwa, baada ya kutokea kwa ajali ya mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso, usiku wa kuamkia siku ya Jumatano.
Polisi wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo mbaya katika barabara kuu ya kutoka Kampala kwenda Gulu, Kaskazini mwa nchi hiyo, kupitia ukurasa wake wa X.
“Mabasi hayo mawili yamegongana uso kwa uso, wakati yakijaribu kupishana” ripoti ya polisi imesema.
Magari mengine manne yamehusika pia kwenye ajali hiyo, ambapo yalipoteza mwelekeo na kubingiria mara kadhaa.
“Tumepoteza watu 46 na wengine wamejeruhiwa” Taarifa ya polisi ilieleza, baada ya idadi ya awali ya 63 kubadilishwa.
Waliojeruhiwa, wamepelekwa katika hospitali ya Kiryandongo kupewa matibabu huku, idadi yao ikiwa haijafahamika vema.
Uganda ni miongoni mwa nchi za Afrika, zinazokabiliwa na ongezeko la ajali kwa sababu ya ubovu wa barabara, uchovu wa madereva, madereva kukosa umakini barabarani na mwendo kasi.
Mwezi Aprili mwaka huu, watu 10 walipoteza maisha Magharibi mwa nchi hiyo, baada ya basi, walilokuwa wanasafiria, kukosa mwelekeo barabarani.
Aidha, wachuuzi 20 walipoteza maisha baada ya lori, lililokuwa linawasafirisha kupata ajali mwezi Agosti.
Uganda imeshuhudia ajali 4,434, zilizosababisha vifo 5,144, kwa mujibu wa takwimu za serikali kuhusu usalama barabarani kwa mwaka 2024.