Meneja wa Napoli, Antonio Conte amelalamikia mipango mibovu ya usajili kwa timu yake akidai imechangia kichapo cha mabao 6-2 ugenini kutoka kwa PSV Eindhoven jana katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Conte amesema kuwa usajili ambao haukuzingatia mahitaji ya msingi, unaweza kuwa mwanzo wa kufanya vibaya kwa timu hiyo msimu huu.

Licha ya Scott McTominay kufunga mabao mawili juzi, mambo yalionekana kuwa magumu kwa upande wa Napoli ambayo ilijikuta ikipokea kipigo hicho kizito.

Na kimekuwa kichapo cha pili mfululizo kwa Napoli baada ya Jumamosi iliyopita kuchapwa bao 1-0 na Torino katika Ligi Kuu Italia.

Conte ana wasiwasi kwamba mabadiliko mengi ambayo yamefanywa katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi linaweza kuiweka Napoli katika wakati mgumu na kuhatarisha kibarua chake.

“Mwaka jana tulishinda ubingwa wa kipekee na wa aina yake ambao kila mmoja alijituma katika kiwango cha juu sana tukiwa na umoja na umoja katika bodi. Mwaka huu hata hivyo, katikati ya kucheza mechi nyingi na kuingiza wachezaji wengi.

“Kwa maoni yangu, wachezaji tisa wapya ni wengi. Hatukuwa na balansi. Nimekuwa nikisema mwaka huu ni mgumu. Kuna baadhi ya vitu vinatakiwa kunyonywa baada ya muda.

“Hii ni ngazi ya Ligi ya Mabingwa. Tuna machache ya kusema na tuna mengi ya kufanyia kazi kubwa. Wote tunatakiwa kukitengeneza kile tulichokuwa nacho msimu uliopita,” amesema Conte.

Miongoni mwa sajili ambazo Napoli walizifanya katika majira ya kiangazi ambazo zimekuwa zikikosolewa ni ya Kevin De Bruyne na Rasmus Hojlund.

De Bruyne alijiunga na Napoli kutoka Manchester City na Hojlund alitokea Manchester United.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *