Barcelona imeendelea kutisha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Olympiacos mabao 6-1 kwenye Uwanja wa Estadi Olímpic Luís Companys, Hispania. Fermin Lopez alikuwa shujaa wa mechi hiyo akifunga hat-trick, huku Marcus Rashford akiendeleza ubora wake kwa kufunga mabao mawili, na Lamine Yamal akihitimisha kwa penalti.

Barcelona ilianza kwa kasi, Lopez akifunga mabao mawili kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza la tatu kipindi cha pili. Olympiacos walipata bao pekee kupitia penalti ya Ayoub El Kaabi, lakini matumaini yao yakazimwa baada ya Santiago Hezze kuonyeshwa kadi nyekundu.

Yamal, mwenye umri wa miaka 18, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mechi 25 za Ligi ya Mabingwa na kufunga bao la penalti. Rashford alipachika mabao mawili ya kuvutia, akifikisha manne katika mechi tatu za michuano hiyo.

Ushindi huo wa 6-1 ni mkubwa zaidi kwa Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2017 ilipoifunga PSG kwa matokeo kama hayo. Mabingwa hao wa Hispania sasa wana alama sita baada ya mechi tatu, huku Olympiacos ikiendelea kulemewa ikiwa na pointi moja pekee.

Arsenal imefunga mabao manne ndani ya dakika 14 pekee ilipoichapa Atletico Madrid 4-0 na kuendeleza mwanzo wao mzuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ikichezwa usiku wa Oktoba 21, 2025 Uwanja wa Emirates, England.

Kipindi cha kwanza kilikuwa na tahadhari nyingi, hali ambayo iliendelea mwanzoni mwa kipindi cha pili huku mashabiki wakijiuliza bao la kwanza lingeanzia wapi.

Beki wa kati, Gabriel Magalhães alijibu swali hilo alipofunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa kwa ustadi na Declan Rice dakika ya 57.

Bao hilo lilianzisha maafa kwa Atletico, kwani Arsenal iliwafanya wapinzani wao ambao kwa kawaida ni wagumu, kuteseka vilivyo.

Gabriel Martinelli aliongeza bao la pili kwa shuti la ustadi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Myles Lewis-Skelly, kabla ya mshambuliaji Viktor Gyökeres kufunga bao lake la kwanza baada ya mechi nane akiwa na Arsenal.

Mshambuliaji huyo raia wa Sweden, alipachika bao lake la pili dakika tatu baadaye akimalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Gabriel Magalhães kufuatia kona nyingine hatari ya Arsenal.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Arsenal imeshinda mechi zake tatu za kwanza za mashindano hayo msimu huu kiwa haijaruhusu bao huku yenyewe ikifunga manane.

Arsenal imefikisha pointi tisa, sawa na PSG na Inter Milan zinazoshika nafasi ya kwanza na pili kwa tofauti ya mabao baada ya kucheza mechi tatu.

Washika bunduki hao wa London wanaokamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa michuano hiyo, inakuwa timu pekee sambamba na Inter Milan ambazo hazijaruhusu bao hadi sasa kati ya timu 36 shiriki.

Erling Haaland ameendelea na rekodi yake ya kufunga alipofumania nyavu kwa mara ya 12 mfululizo, akiisaidia Manchester City kumaliza ukame wa ushindi ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuibuka na ushindi wa mabao 0-2 dhidi ya Villarreal.

Fowadi huyo wa Norway, ameonyesha kiwango cha ajabu msimu huu, akiwa amefunga mabao 24 katika mechi 14 za klabu na timu ya taifa, huku City ikipata alama tatu ugenini barani Ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

Kikosi cha Pep Guardiola kilitawala kipindi cha kwanza, na nahodha Bernardo Silva aliongeza bao la pili kabla ya mapumziko kwa kichwa kizuri baada ya kupokea krosi ya Savinho.

Man City imefikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, imeshinda mbili na sare moja, imefunga mabao sita na kuruhusu mawili huku ikishika nafasi ya katika msimamo wa michuano hiyo.

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain wametoa onyo kali baada ya kuibamiza Bayer Leverkusen mabao 2-7 na kufikisha ushindi wa tatu mfululizo katika michuano hiyo.

Katika mechi hiyo iliyochezwa BayArena, Desire Doue alifunga mara mbili, huku Willian Pacho na Khvicha Kvaratskhelia wakiongeza mabao mengine kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika na PSG kuongoza 4-1. Nuno Mendes, mshindi wa Ballon d’Or Ousmane Dembele na Vitinha walikamilisha kipigo hicho kikali.

Beki Willian Pacho aliipa PSG bao la kuongoza dakika ya saba baada ya kukutana na krosi murua ya Nuno Mendes. Dakika 16 baadaye, Leverkusen ilipata penalti baada ya Illia Zabarnyi kumchezea rafu Claudio Echeverri.

Hata hivyo, mkwaju wa Alejandro Grimaldo uligonga mwamba, na dakika saba baadaye nahodha wa Leverkusen, Robert Andrich, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya VAR kubadilisha kadi ya njano kufuatia kumgonga Doue usoni kwa kiwiko.

Faida ya kuwa na mchezaji mmoja zaidi haikudumu muda mrefu kwa PSG, kwani Zabarnyi naye alitolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumuangusha Christian Kofane ndani ya eneo la penalti.

Mashabiki wa Leverkusen walishangilia Aleix Garcia alipofunga penalti hiyo, lakini furaha yao haikudumu. Ndani ya dakika tano pekee, Doue alifunga kwa mkwaju wa chini uliopinda, Kvaratskhelia akaongeza kwa shuti lililogonga miamba yote miwili kabla ya kuingia wavuni, na Doue akamalizia shambulizi la kushtukiza kwa mkwaju wa kupinda.

Kipindi cha pili kilianza kwa mtindo huohuo, Vitinha alipenya katikati ya safu ya kiungo ya Leverkusen na kumpasia Mendes aliyemalizia kwa ustadi kwenye lango la Mark Flekken.

Garcia alipunguza bao kwa shuti kali la umbali wa yadi 30 lililopaa hadi kona ya juu ya lango, lakini Dembele, aliyekuwa amerudi kutoka kuuguza majeraha ya misuli, aliifungia PSG bao la sita dakika tatu tu tangu aingie uwanjani.

Vitinha alikamilisha bao la saba dakika ya 90, akipiga shuti la chini lililokwenda moja kwa moja kwenye kona ya lango.

PSV Eindhoven imepindua matokeo kwa kishindo na kuishangaza Napoli iliyomaliza ikiwa na wachezaji 10, kwa ushindi wa mabao 6-2 katika ukiwa ni ushindi wao wa kwanza msimu huu.

Scott McTominay alianza kufunga na baadaye akapata bao la kufutia machozi kwa Napoli katika mechi iliyojaa matukio iliyopigwa Uwanja wa Philips, Uholanzi.

Dakika saba tu baada ya bao la ufunguzi la McTominay, PSV ilikuwa imeshaongoza baada ya Ismael Saibari kufunga bao zuri kufuatia bao la kujifunga la Alessandro Buongiorno.

Dennis Man aliongeza mabao mawili kwa wenyeji, kila moja likitokea kabla na baada ya Lorenzo Lucca kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 76 kwa kumkosoa mwamuzi.

McTominay, ambaye aling’ara sana msimu wake wa kwanza akiwa na Napoli, alipunguza tofauti kwa bao dakika tano kabla ya muda wa kawaida kumalizika.

Hata hivyo, PSV ilijibu haraka kupitia Ricardo Pepi aliyerejesha pengo la mabao matatu, kabla ya Couhaib Driouech kufunga bao maridadi la mbali na kukamilisha usiku bora kwa wenyeji.

Ni kipigo cha pili mfululizo kwa kikosi cha Antonio Conte, ambacho kilipoteza nafasi ya kuongoza Serie A Jumamosi iliyopita baada ya kuchapwa na Torino.

Napoli sasa inashika nafasi ya 22 kati ya timu 36 katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, huku PSV ikipanda hadi nafasi ya 11.

Jobe Bellingham ametoa mchango wake wa kwanza tangu ajiunge na Borussia Dortmund baada ya kusaidia bao la ufunguzi la Felix Nmecha, ambaye alifunga mara mbili na kuisaidia klabu hiyo ya Ujerumani kushinda 2-4 ugenini dhidi ya Copenhagen kwenye Uwanja w Parken, Denmark.

Bellingham amekuwa akipata dakika chache za kucheza kwenye Bundesliga tangu alipohamia Dortmund kwa pauni milioni 27 akitokea Sunderland majira ya kiangazi, lakini alitumia vizuri nafasi yake katika mechi yake ya pili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutoa pasi ya bao.

Mshambuliaji Mjerumani, Nmecha alipokea pasi safi kutoka kwa Bellingham dakika ya 20 na kupiga shuti kali kutoka pembezoni mwa eneo la hatari lililojaa nguvu na usahihi.

Copenhagen ilisawazisha katika mazingira ya kuchekesha kwani mlinda mlango Gregor Kobel aliokoa shuti la chini kufuatia kona, lakini jitihada za Ramy Bensebaini za kuondoa hatari, mpira ulimgonga beki mwenzake Waldemar Anton na kuingia wavuni.

Bensebaini alijirekebisha dakika ya 61 kwa utulivu mkubwa alipofunga penalti baada ya Serhou Guirassy kuchezewa vibaya ndani ya eneo la hatari.

Nmecha aliongeza bao la tatu dakika ya 76 baada ya shuti lake kuguswa na beki na kumfanya kipa wa Copenhagen, Dominik Kotarski, ashindwe kuelekea upande sahihi.

Bellingham alionekana kuwa na hamu kubwa ya kufunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo, lakini ni Fabio Silva, aliyewahi kuchezea Wolves, aliyeongeza bao la nne mwishoni mwa mechi.

Viktor Dadason alipunguza tofauti kwa bao la kufutia machozi dakika za lala salama baada ya mpira wake wa kichwa kuvuka mstari.

Dortmund sasa itasafiri kuifuata Manchester City Novemba 5, 2025 ikiwa na pointi saba baada ya mechi tatu, huku Copenhagen ikibaki bila ushindi baada ya sare na Bayer Leverkusen na kupoteza 2-0 dhidi ya Qarabag.

Harvey Barnes na Anthony Gordon wameipa Newcastle United ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Benfica inayoongozwa na Jose Mourinho katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ikichezwa St James’ Park.

Gordon, ambaye hakuwa akilindwa, alifungua ukurasa wa mabao kipindi cha kwanza kwa kutuliza mpira na kuumimina wavuni akimshinda kipa wa Benfica, Anatoliy Trubin, baada ya kupokea pasi ya Jacob Murphy iliyopita mbele ya lango.

Hilo lilikuwa bao la nne kwa Gordon katika mechi tatu za mashindano hayo na likawapa Newcastle motisha ya kusaka mengine zaidi kipindi cha pili.

Barnes aliongeza bao la pili baada ya kipa Nick Pope kutupa mpira mrefu kuelekea upande wa kulia.

Beki wa Benfica, Antonio Silva, alikosea kuumudu mpira huo na Barnes akauwahi, kisha akafunga kwa mpira uliogonga mwamba kabla ya kuingia wavuni.

Kabla ya filimbi ya mwisho, Barnes alipachika bao la tatu na kukamilisha ushindi baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Gordon, kisha akampiga chenga kipa Trubin na kupenyeza mpira kupitia miguu yake.

Benfica itasikitika kwa nafasi ilizopoteza, kwani ilikaribia kufunga mara mbili kipindi cha kwanza, Pope akiuokoa mkwaju wa Dodi Lukebakio kwa mkono, kisha Lukebakio huyo huyo akagonga mwamba dakika chache baadaye kwa shuti kali kutoka nje ya boksi.

Hata hivyo, Gordon na Barnes waliitumia vyema kila nafasi waliyopata, na Newcastle ikaandika historia ya kupata ushindi wa pili mfululizo katika Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2003 na kufikisha pointi sita ikikamata nafasi ya saba kwenye msimamo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *