Wanajeshi wawili wa Rwanda wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuwaunga mkono waasi wa Machi 23 (M23) waliofanya mashambulizi mapema juzi Jumatatu dhidi ya kambi za kijeshi za serikali huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hayo yamesemwa na Jeshi la DRC (FARDC) na kuongeza kuwa: Maeneo kadhaa ya FARDC yameshambuliwa na waasi M23 kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa saa za eneo la Rutshuru, kaskazini mwa mji wa Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Katika kikao na waandishi wa habari, Jenerali Sylvain Ekenge, msemaji wa gavana wa Kivu Kaskazini, amethibitisha kuwa wanajeshi wawili wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) walikamatwa wakati wa mashambulizi hayo. Aidha akaishutumu Rwanda kwa kula njama na waasi wa M23 za kushambulia kambi za kijesi za serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Aidha amesema: “M23, wakiungwa mkono na Wanajeshi wa Rwanda, walivamia na kushambulia maeneo ya FARDC” katika eneo la Rutshuru.

Hii ni mara ya tatu tangu Oktoba 2021 kwa Jeshila DRC kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 katika mashambulizi haya dhidi ya maeneo ya kijeshi ya DRC kwenye eneo la Rutshuru.

M23 ni kundi la waasi ambalo zamani lilikuwa likiitwa National Congress for the Defence of the People (CNDP) jina hilo la M23 lilianzakutumia tarehe 23 Machi 2009.

Kwa upande wao viongozi wa M23 wanailalamikia serikali ya DRC wakidai kuwa haihesimu makubaliano ya kusimamisha mapigano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *