
COASTAL Union imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Fountain Gate kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga.
Fountain ilikuwa ya kwanza kupata bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa Juma Abushiri ‘Chuga’ aliyepiga shuti la taratibu lililomshinda kipa wa Coastal Union, Wilbol Maseke.
Hadi kipindi cha kwanza kinatamatika Fountain Gate ilikuwa inaongoza bao moja.
Kipindi cha pili Coastal Union walionekana kubadilika tangu mechi inaanza wakishambulia kwa nguvu lango la Fountain.
Dakika ya 60 Coastal Union ilisawazisha bao kwa mkwaju wa penayti kupitia kwa Makambo Jr ambaye alipiga mara ya kwanza mpira ukaokolewa na kipa Parapanda wa Fountain, lakini ukamshinda kujaa mikononi ulipomtoka.
Kwa matokeo hayo yanaifanya Coastal kusalia nafasi ya saba na pointi tano kwenye mechi tano ilizocheza ikishinda moja, sare mbili na kupoteza mbili.
Fountain ambayo imeambulia ushindi mara moja, sare moja na kupoteza tatu inasalia nafasi ya 14 ikiwa na pointi nne.
Akizungumza baada ya mechi kutamatika kocha wa Coastal Union, Mohamed Muya amesema bado timu ni mpya, lakini wana kazi ya kufanya hasa kwenye eneo la umaliziaji.
“Bado timu haina maelewano makubwa eneo la mwisho tumekuwa tukifanyia kazi mazoezini, lakini naamini tutakuwa sawa,” amesema Muya.
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Lazier amesema lengo lao ilikuwa kupata pointi tatu, lakini bahati haikuwa upande wao wameambulia moja.
“Tulikuwa vizuri lakini kuna baadhi ya makosa madogo tumeyafanya tukasababisha penalti. Tunaenda kurekebisha mazoezini na tutarudi kuwa imara zaidi,” amesema.
Kikosi cha Fountain Gate kilichoanza: Rashid Parapanda, Jimson Mwanuke, Obinna Awara
Jackson Shiga, Derick Mukombozi, Daniel Joram, Elie Mkono, Ismail Aziz Kada, Joshua Mwakasaba, Shomari Mponzi na Juma Abushiri.
Kikosi cha Coastal Union: Wilbol Maseke, Ally Ayubu, Boniface Mkandala, Athuman Masumbuko ‘Makambo Jr’, Gradi Lassa, Godfrey Balugu, Aidan Rasmus, Suleiman Saleh, Ali Said, Ally Ramadhan na Msimu.