
Operesheni ya kiintelijensia ya Iran iliyofanyika kwa mafanikio, imefichua waliko watu wanaohusika na shirika la kijasusi la Israel Mossad, ambao waliwatumikia maadui hasa Israel na Marekani wakati wa vita vya upashaji habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu Iran.
Taarifa hiyo ilitangazwa jana kwenye Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na kuonesha jinsi maafisa wa ujasusi wa Iran walivyogundua makazi hasa ya mamluki walioajiriwa moja kwa moja na wale wanaoonekana mara kwa mara katika televisheni ya Israel inayojiita “Iran International.”
Ripoti hiyo iliyotangazwa jana kwenye kanali mbalimbali za televisheni za Iran imeonesha picha na maelezo ya maficho halisi ya watu hao katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel ikiwemo Tel Aviv.
Watu hao ni pamoja na Babak Es’haghi, mmoja wa waandishi wa televisheni hiyo ya Kizayuni ambaye amegundulika mahali alipo kuwa ni Mtaa wa Fabregat katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Holon karibu na Tel Aviv.
Mwingine aliyetangazwa kwenye kipindi hicho cha televisheni ni Meir Javedanfar, ambaye huwa anahojiwa mara kwa mara na televisheni ya Israel inayojiita “Iran International” na ambaye anaukingia kifua mno utawala wa Kizayuni na jinai zake kubwa. Maficho yake yamegunduliwa na kuoneshwa kwenye kipindi hicho cha televisheni yakiwa ndani ya mji wa Tel Aviv.
Operesheni hiyo ya kiintelijensia ya Iran imefichua pia jengo zima lililoko kwenye Mtaa wa Degania huko Holon ambako ndiko wanakokaa wafanyakazi wa televisheni ya Kizayuni inayojiita Iran International.
Katika muda wote wa ukatili wa utawala wa Kizayuni na washirika wake, ikiwa ni pamoja na mauaji ya umati ya Israel ya miaka miwili huko Ghaza na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, muda wote huo televisheni hiyo ya Israel inayorusha matangazo kwa lugha ya Kifarsi, ilikuwa mstari wa mbele kuhalalisha jinai za Wazayuni na kuchochea jinai zaidi.