Wizara hiyo ya Afya imesema kwa ujumla miili 57 iliyorejeshwa Gaza kutoka Israel, imetambuliwa na jamaa zao huku miili mingine 54 ambayo haikutambuliwa imezikwa leo Jumatano katika makaburi ya Deir el-Balah.
Shirika la ulinzi wa raia la Gaza,limesema msafara wa maziko ulianzia katika hospitali ya Nasser kusini mwa mji wa Khan Yunis kuelekea katika makaburi hayo yalioko katikati mwa Gaza.
Vidio za shirika la habari la AFP kutoka hospitali hiyo, zilionyesha miili kadhaa ikiwa sakafuni imefunikwa kwa mifuko myeupe maalum ya kubebea maiti huku makundi ya watu yakisimama nyuma ya miili hiyo kwa maombi.
Raia mmoja wa Gaza kwa jina Umm Hassan Hammad alisema hakuweza kuutambua mwili wa mtoto wake wa kiume aliyetoweka tangu Oktoba 7 siku ambayo wanamgambo wa Hamas walivamia kusini mwa Israel, tukio lililochochea mzozo wa sasa wa Mashariki ya Kati, ambao umeendelea kwa zaidi ya miaka miwili.
“Kila siku ninakuja hapa, kwa matumaini naweza kumtambua kwa nguo zake alizovaa tangu Oktoba 7 lakini kwa bahati mbaya sijammpata.”
Vance: Kuna kazi kubwa ya kufanywa kwa mpango wa amani ya Gaza
Chini ya mpango wa amani ya Gaza uliopendekezwa na rais wa Marekani Donald Trump, Israel ilipaswa kutoa miili 15 ya wapalestina, kwa kila mwili wa mateka wake mmoja utakaorejeshwa kutoka Gaza.
Awali jeshi la Israel lilisema limetambua miili miwili ya mateka iliyorejeshwa kutoka huko kuwa ya Aryeh Zalmanovich na Tamir Adar.
Tangu kutekelezwa makubaliano ya usitishaji mapigano mnamo Oktoba 10 mwaka huu, mabaki ya mateka 15 kati ya 28 waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo wa Kipalestina yamerudishwa Israel.
Kwengineko Makamu wa rais wa Marekani JD Vance ametahadharisha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa kuelekea utekelezwaji kikamilifu wa mpango wa amani ya Gaza. Aliyasema hayo baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika siku ya pili ya ziara yake Israel.
“Tuko hapa kuzungumzia amani. Tuko hapa kuzungumzia namna ya kuhakikisha makubaliano ya amani ni imara ili tuelekee katika awamu ya pili na ya tatu kwa mafanikio. Kama Rais Herzog alivyosema kutakuwa na changamoto, mambo yatakuwa magumu lakini nina matumaini makubwa hasa baada ya kuzungumza na Israel na rafiki zetu wa Ghuba kwamba inawezekana Inawezekana kwa rafiki zetu wa Israel na wale wa Ghuba kujenga Mashariki ya Kati iliyo bora zaidi kwa kila mtu.”
ICJ yasema Israel ihakikishe mahitaji muhimu yanafika Gaza
Wakati huo huo Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa (ICJ)imesema Israel ina wajibu wa kuhakikisha mahitaji muhimu ya watu wa Gaza yanatimizwa.
Majaji 11 wa ICJ walisema Israel inalazimika kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kutoa misaada Gaza na viunga vyake pamoja na kuliunga mkono pia shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.
Majaji hao wameongeza kuwa hadi sasa Israel haijathibitisha iwapo baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA ni wanachama wa kundi la Hamas kama ilivyodai awali.
Haya yanajiri wakati Uturuki na Qatar wakiendeleza juhudi za kuulinda mpango wa amani ya Gaza huku viongozi wao rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani. wakkikutana Doha. hili linaendelea wakati Benjamin Netanyahu akiwa na mashaka ya Uturuki kuchangia majeshi yake kupelekwa Gaza.