fvc

Chanzo cha picha, GAVRIIL GRIGOROV/POOL/AFP

    • Author, Paul Kirby
    • Nafasi, Mhariri wa masuala ya Ulaya

Ikiwa Rais Vladimir Putin wa Urusi atakwenda Budapest, Hungary kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani, katika wiki mbili zijazo, atalazimika kuondoa vizuizi vichache kwanza.

Putin aliposafiri hadi Alaska kwa ajili ya mkutano wake mwezi Agosti, Marekani ilitoa ruhusa maalum kwa ndege ya rais huyo iliyopewa jina la “Flying Kremlin” ambayo ina injini nne na imejaa mifumo ya ulinzi.

Ndege za Urusi zimepigwa marufuku kupita anga la Marekani, na anga la Umoja wa Ulaya pia. Kwa hivyo ikiwa Putin atakwenda Budapest atahitaji ruhusa maalum kuruka juu ya nchi mwanachama wa EU.

Hungary isiyo na bandari si eneo rahisi kufikia kwa rais wa Urusi ambaye mara chache sana anatembea nje ya nchi na hajasafiri kwenda Umoja wa Ulaya kwa miaka.

“Kwa sasa haijulikani atasafiri vipi,” anasema msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov. “Tunachojua ni nia ya marais kufanya mkutano.”

Siku chache baada ya Putin kuamuru uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Februari 2022, Umoja wa Ulaya, EU ilizuia mali za kiongozi huyo na Waziri wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov.

Pia unaweza kusoma
Viktor Orban wa Hungary ni mmoja wa washirika wa karibu wa Putin barani Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images

Marufuku pia iliwekwa kwa ndege zote za Urusi kutoruka katika anga ya nchi zote 27 za EU. Hungary na majirani zake ni nchi wanachama wa Nato pia.

Putin pia anatuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa uhalifu wa kivita wa kuwaondosha na kuwahamisha watoto wa Ukraine na kuwapeleka nchini Urusi kinyume cha sheria.

Ingawa Hungary inaamini hayo yanaweza kutatuliwa. Nchi hiyo iko katika harakati za kujiondoa ICC.

Putin na rais Viktor Orban wa Hungary, mshirika wake wa karibu katika Umoja wa Ulaya, pengine tayari wamejadili mkutano huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary Peter Szijjarto amewaambia waandishi wa habari “bila shaka tutahakikisha anaweza kuingia Hungary, kufanya mazungumzo yenye mafanikio, na kisha kurejea nyumbani.”

Umoja wa Ulaya unasemaje?

Tume ya Umoja wa Ulaya imesema mkutano wowote wa “haki na amani ya kudumu kwa Ukraine” unakaribishwa na inaunga mkono juhudi za Rais Trump kufanikisha hilo. Na imesema hakuna marufuku ya kusafiri kwa Putin, ni kushikilia mali tu.

Jambo kubwa ni jinsi kiongozi wa Urusi atakavyosafiri kutoka Moscow hadi Budapest. Ni wazi kuwa hatanunua tiketi ya ndege ya abiria ya Air Serbia kwenda Belgrade au kupanda treni hadi Hungary, ambayo inaweza kuwa njia ya moja kwa moja.

Atataka kupanda ndege yake ya Il-96 ili kuhakikisha usalama wake, lakini hilo litamaanisha kutumia anga ya nchi wanachama wa EU na Nato na kupata kibali cha kuvunja marufuku ya EU kwa ndege za Urusi.

Msemaji wa Tume ya Umoja wa Ulaya Anitta Hipper alisema siku ya Ijumaa kwamba “katika suala la safari, nchi wanachama zinaweza kutoa kibali cha dharau lakini lazima kitolewe na nchi wanachama wenyewe.”

Nato pia imelielekeza suala hilo kwa mamlaka husika za kitaifa, na kwa kuwa Trump anahusika basi nchi hizo zinaweza kuridhia.

Atapita wapi?

Ndege ya Putin ya Ilyushin imepewa jina la "Flying Kremlin"

Chanzo cha picha, Getty

Hata ikiwa kutakuwa na ruhusa, kwa kuangalia ramani kunaonyesha Putin anaweza kulazimika kuchukua njia ya mzunguko. Hawezi kupita Ukraine, na pengine hawezi pia kupita Poland kwa sababu ya mahusiana baridi na Moscow.

Labda njia ya moja kwa moja ni kupita pwani ya mashariki ya Bahari Nyeusi na Uturuki, kisha kupitia Bulgaria na Serbia au Romania hadi Hungary.

Rais wa Serbia, Aleksandar Vucic, anamfahamu Putin vyema na Air Serbia ina safari za moja kwa moja hadi Moscow kupitia anga ya Umoja wa Ulaya. Serbia inataka kujiunga na EU lakini bado si mwanachama.

Ni nchi za Umoja wa Ulaya, Bulgaria au pengine Romania, ambazo zitalazimika kutoa kibali, na watalazimika kuisindikiza ndege ya Putin kupitia anga yao.

Romania ina kile kinachotarajiwa kuwa kambi kubwa zaidi ya Nato barani Ulaya, na Bulgaria pia inajenga kambi ya Nato kama sehemu ya juhudi za kuimarisha muungano huo wa kujihami kwa upande wa mashariki.

Msemaji wa Bucharest ameiambia BBC, “Romania bado haijapokea ombi kutoka Shirikisho la Urusi la kutumia anga yake.”

Ikiwa Putin anataka kusafiri kwa usalama zaidi, anaweza kuruka kupitia Uturuki, kuzunguka pwani ya kusini ya Ugiriki na kisha kupitia anga ya Montenegrin kabla ya kuvuka Serbia. Lakini ni njia ndefu zaidi.

Budapest sio eneo rahisi, hata ikiwa mkutano huo ni jambo zuri kwa Viktor Orban, ambaye kwa muda mrefu amekuwa na uhusiano mzuri na Putin na Donald Trump.

Kuhusu Orban, rais Trump amesema, “ni kiongozi ambaye tunampenda,” alisema siku ya Ijumaa, “Putin anampenda, nami nampenda.”

Ndani ya saa chache baada ya Budapest kutajwa kama mwenyeji, Orban alimpigia simu Putin na akatangaza kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Maandalizi yanapamba moto!”

Amekuwa mwepesi kuweka wazi kuwa Umoja wa Ulaya, hautahusika na mazungumzo hayo.

“Kwa kuwa EU inaunga mkono vita, ni jambo la busara ikaje nje ya mchakato huu wa amani,” aliiambia redio ya Hungary siku ya Ijumaa.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *