Leo ni Jumanne tarehe 28 Mfunguo Saba Rabiul Thani 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Oktoba mwaka 2025.
Miaka 809 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibnul Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus.
Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad, na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa.
Ibn Arabi alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya “Tafsir Kabir”, “al-Futuhatul Makkiyyah” na “Fususul Hikam”.

Siku kama ya leo miaka 235 iliyopita, alizaliwa malenga wa Kifaransa, Alphonse de Lamartine.
De Lamartine alitambulika kuwa msanii na mwanafikra mkubwa nchini Ufaransa. Aliwahi pia kusafiri Mashariki na kuishi katika mji mkuu wa Lebanon, Bairut. Aidha miongoni mwa athari za malenga huyu, ni pamoja na “Safari ya Mashariki” na “Kimya cha Malaika”.
Alphonse de Lamartine alifariki dunia mwaka 1869.

Miaka 192 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite.
Nobel alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza sayansi ya kemia na baadaye akafanya utafiti mkubwa katika uwanja huo na kufanikiwa kuvumbua mada za mlipuko yaani (dynamite). Kinyume na alivyotarajia, majeshi ya nchi mbalimbali yalianza kutumia dynamite vitani na hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi.
Mkemia Nobel ambaye alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na amani.
Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii Tuzo ya Amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Somalia ilipata uhuru na siku hii inajulikana nchini humo kama Siku ya Taifa.
Kijiografia Somalia ipo kaskazini mashariki mwa bara la Afrika katika eneo linalojulikana kama Pembe ya Afrika. Mji mkuu wa Somalia ni Mogadishu na lugha rasmi ya nchi hiyo ni Kisomali na Kiarabu. Asilimia 99 ya wananchi wa Somalia ni Waislamu.
Nchi hiyo kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya ukoloni wa Italia na Uingereza mpaka ilipojipatia uhuru mwaka 1960 katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala, kamanda Jeshi la Majini la Palestina aliuawa na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala ghasibu wa Kizayuni Mossad.
Wazayuni walimuuwa kigaidi kamanda huyo wa jeshi la majini la Palestina kwa kutega bomu ndani ya gari lake huko Athens mji mkuu wa Ugiriki.
Brigedia Jenerali Abu Ghazala ni miongoni mwa wahanga wa ugaidi wa kiserikali wa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni unaoungwa mkono kwa hali na mali na Marekani.
