Dar es Salaam. Mwonekano wa mtu unatoa picha kwa watu wanaomzunguka kumchukulia kuwa ni mtu wa aina gani. Nje na kuzingatia afya wapo wanaopenda kupungua ili kujihisi vizuri na kuongeza ujasiri wa kuonekana mbele za watu.
Kiafya inashauriwa kilo za mtu ziendane na urefu na hilo limekuwa na mwamko kwa wengi wakiwemo mastaa ambao walikuwa na miili mikubwa na sasa wamepungua kwa kufanya mazoezi na au kupunguza milo ili kuepukana na magonjwa, huku pia wakizingatia mvuto.
Mwananchi linakuletea baadhi ya mastaa waliokuwa na miili minene na sasa wamejipunguza, huku baadhi wakidai hali hiyo inawajengea kujiamini na kujihisi vizuri kiafya.
Ukiondoa waliopungua wapo waliokuwa wembamba na sasa ni ‘vibonge’, ilhali kuna wanaoonekana katika gym wakiwa katika haraka za kuondoa uzito na kutengeneza mwonekano wenye mvuto mbele ya mashabiki wao.
TABU MTINGITA
Mchekeshaji Tabu Mtingita anazungumzia hilo akisema: “Unene unazeesha. Nilipotoka Mtwara kuja Dar es Salaam mwili ulijaa. Nilikuwa napumua hovyo, nakoroma, nyonga zilikuwa zinanishika nikienda hospitali kupima UTI sina. Pingili za mgongo zilikuwa zinagoma, ukilala ni staili moja hiyo hiyo. Nimepungua kwa sababu nafanya ‘dayati’ nimeacha vitu vitamu na kuna dawa natumia kwa sasa ni mwepesi. Najiamini na kujihisi vizuri.
Anaongeza: “Kabla ya kupungua nilikuwa nakula chipsi sahani tatu na mayai sita ila kwa sasa sili kabisa hivyo vitu. Nimepungua nikivaa nguo napendeza. Nimekuwa binti na najiamini mbele za watu na siumwi tena. Kinachonisumbua ni pumu ambayo nilikuwa nayo tangu zamani na inanibana mara chache.
“Nilikuwa na kilo 127 kwa sasa nacheza na 80 wakati mwingine 70 na bado naendelea kupungua nifike hadi 60. Nawashauri wanawake wenzangu wasijichakaze na kujichosha kutokana na uzito mkubwa. Kwanza ukipungua ni rahisi kufanya kazi kwa haraka bila kuchoka.”
WEMA SEPETU
Mwaka 2006 alipoibuka mshindi wa Miss Tanzania alikuwa mwembamba, lakini baada ya miaka kadhaa akawa mnene na mashabiki zake wakaanza ‘kumng’ong’a kwa mwonekano aliokuwa nao.
Mwaka 2018 Wema alianza kupungua taratibu na sasa amerudi kwenye mwonekano wake wa zamani uliompa taji la urembo na aliwahi kulizungumzia hilo katika mahojiano aliyowahi kufanya.
“Unene ni mbaya, najisikia mwepesi na nikivaa nguo napendeza ingawa huwa nawashangaa watu wanaoona nilivyopungua, nimekuwa mbaya wamenisahau nilipokuwa nachukua taji mwaka 2006 nilikuwaje,” anasema.
IDRIS SULTAN
Mwigizaji na mshindi wa Big Brother Hotshots mwaka 2014 Idris Sultan ameonekana kupungua zaidi tofauti na mwanzo, jambo lililowashangaza baadhi ya mashabiki wake. Wapo wengine wanaonyesha wasiwasi kuona huenda kuna kitu kinamsumbua, ingawa upande wake anaona ni kitu cha kawaida.
Aliulizwa na wanahabari kuhusiana na hilo akajibu: “Kwani kupungua ni kitu kibaya, sipendi kuzungumzia vitu ambavyo siyo vya msingi. Ukitaka kufuatisha mambo ya watu utapata mawazo ndiyo maana jambo hilo linawatatiza wanawake wengi na kufanya maamuzi ya sajali.”
Anaongeza: “Mimi ni mwigizaji siwezi kusema kila kitu wakati huu kwamba labda kuna kazi inakuja mbele yangu. Utakapofika muda sahihi naweza nikaliongelea hilo ama watu wakaja kuona kwa macho yao. Kifupi sina shida kabisa na mwonekano wangu wa sasa.”
Msanii wa filamu, mwanamuziki na mtangazaji anayejulikana kwa jina la Mimi Mars mwonekano wake mpya wa kupungua umewashangaza baadhi ya mashabiki waliokuwa wanaukubali ule wa mwanzo.
Staa huyo aliposti video katika mtandao wa kijamii wa Instagram akionekana na mwili uliopungua akiwa ananyanyua kifaa cha mazoezi, jambo ambalo baadhi ya mashabiki walitoa maoni na kuona alipendeza zaidi na mwili wake wa mwanzo.
RIYAMA ALLY
Msanii wa Bongo Move, Riyama Ally tofauti na kipindi cha nyuma alikuwa anaonekana kibonge, lakini sasa amepungua na wengi wanamsifia katika mtandao wa kijamii wa Instagram anakoposti picha za mwonekano wake.
GIGY MONEY
Msanii wa Bongofleva maarufu kama Gigy Money wakati anaanza muziki wake na kipindi anatangaza alikuwa na mwonekano wa ‘ubonge’ tofauti na sasa ambapo amekuwa ‘modo’.
JACOB STEPHEN ‘JB’
Msanii wa Bongo Move, alimaarufu kama JB mwonekano wake wa sasa ni tofauti amepungua na kuwa na mzuri zaidi. JB mara kadhaa anaonekana yupo gym akifanya mazoezi na wakati mwingine kuogelea ambako inaelezwa kuwa kunasaidia kupunguza mwili.
Kwa sasa msanii wa Bonge Move, Asha Boko anaonekana kupungua na aliwahi kulizungumzia hilo kwamba: “Nafanya ‘dayati’ kwa kuzingatia ushauri wa daktari. Najiona mwepesi na hilo linasaidia kuwa na afya njema na imara kwani sichoki kama ilivyokuwa awali ambapo mwili ulikuwa unapata uchovu wa mara kwa mara.”
REHEMA CHALAMILA
Mkongwe wa Bongofleva alimaarufu kama Ray C aliyewahi kutamba na nyimbo kama Wanifuatia Nini na Na Wewe Milele, Watanzania walimfahamu akiwa na mwili mdogomdogo, lakini baadaye akanenepa kabla ya sasa kurejea katika mwili wake mwembamba. Ingawa kipindi alichokuwa amenenepa ni kile alichokuwa anahusishwa na kuwa katika changamoto ya kutumia dawa za kulevya.
Vibonge wa sasa
Kipindi cha nyuma msanii wa muziki na Bongofleva, Zena Mohamed ‘Shilole’ alikuwa mwembamba tofauti na sasa ambapo anaonekana ni kibonge, ingawa anaonekana yupo gym akifanya mazoezi ya kupunguza mwili.
Shilole ukimtazama katika video ya nyimbo zake Nakomaa na Jiji, Say My Name ft Barnaba na nyinginezo alikuwa modo, tofauti kabisa na mwonekano wake wa sasa.
CHID BENZI
Kabla ya msanii wa Bongofleva, Chid Benz kupata changamoto ya dawa za kulevya alikuwa na mwili wa kawaida, lakini baadaye akaja akakonda sana kabla ya kupelekwa ‘soba’ alikorejea akiwa amenenepa.
Kwa sasa Chid anaonekana akifanya mazoezi gym ili kurejesha mwili wake, tofauti na wa sasa ambao amekuwa kibonge.