KOCHA Florent Ibenge, amesema mshambuliaji wa kikosi hicho, Jephte Kitambala, kwa sasa anatakiwa kuwa na mwendelezo wa kufunga hali ambayo itamuongezea kujiamini zaidi.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, ametua Azam msimu huu akitokea Maniema ambapo tayari amefunga mabao mawili yote katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema, kazi kubwa ya mshambuliaji ni kufunga ndio maana hashangai mashabiki kuuliza kuhusu Kitambala wanapoona anashindwa kufanya hivyo.

Alisema kwa sasa muda umefika wa mshambuliaji huyo kuanza kufunga mfululizo kwani hiyo itamuongezea hali ya kujiamini zaidi, lakini pia hayo yote ni mambo yanayohitaji muda.

“Kitambala ni mshambuliaji mzuri, kitu ambacho ninakifurahia kwake ni namna alivyoweza kuunganika na wenzake kwa haraka kuliko nilivyofikiria.

“Kwa sasa hatua nzuri kwake ni kuendelea kufunga zaidi kwa kuwa timu inamruhusu kupata nafasi ya kuweka mabao kambani ukizingatia kuna viungo wazuri.

“Azam ina wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kutengeneza nafasi na hata kuzitumia, ndio maana kila mchezo tumeweza kufunga, hakuna mechi ambayo tumemaliza bila kupata bao,” alisema.

Azam msimu huu katika mashindano yote, imecheza mechi tano ikishinda nne na sare moja, iMEfunga mabao tisa na kuruhusu moja.

Katika Ligi Kuu Bara, imecheza mechi mbili, ikishinda moja na sare moja, huku Kombe la Shirikisho Afrika mechi tatu zote imeshinda.

Katika mabao tisa, wachezaji wa Azam waliofunga ni Feisal Salum (3), Nassor Saadun (2), Jephte Kitambala (2), Pascal Msindo (1) na Yoro Diaby (1).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *