Mkuu wa Jumuiya ya Biashara ya Pamoja ya Iran na Afrika amesema: “bara la Afrika ni hazina iliyofichika ya uchumi wa dunia na fursa kubwa kwa Iran.”
Masoud Barahman, Mkuu wa Jumuiya ya Biashara ya Pamoja ya Iran na Afrika amesisitiza Jumapili katika Jopo la Wataalamu wa Afrika juu ya uwezekano mkubwa wa ushirikiano wa kiuchumi wa bara hilo na kusema: “bara la Afrika ni hazina iliyofichika ya uchumi wa dunia na ni fursa adhimu kwa Iran.”
Akiashiria fursa zinazopatikana kwa Iran katika sekta ya huduma za madini na uhandisi, Brahman ameongeza kuwa: “Barani Afrika, miradi yenye thamani ya zaidi ya dola trilioni elfu moja inaendelea katika maeneo kama vile ujenzi wa mabwawa, nishati mbadala na ukandarasi. Nchi za bara hilo zinakaribisha uwepo wa wataalamu na makampuni ya Iran katika nyanja ya uchimbaji madini, na hata kumekuwa na mwito kwa wanaharakati wa miradi ya dhahabu wa Iran.”
Ingawa bara la Afrika liko nyuma ya mabara mengine katika suala la miundombinu, ukuaji wake wa uchumi ni wa juu kuliko wastani wa kimataifa, na hii inachukuliwa kuwa fursa ya kimkakati kwa Iran kupanua uhusiano wa kibiashara na uwepo wake katika masoko yanayoibukia.
Moja ya mbinu za Iran katika maingiliano na nchi za Kiafrika ni kubadilishana vitu; kwa maana kwamba, badala ya kuuza bidhaa nje, malighafi zinazohitajika na viwanda vya nchi hutolewa. Mtindo huu wa ushirikiano unaweza kuwa njia mwafaka ya kuendeleza maingiliano ya kiuchumi kati ya Iran na bara la Afrika.
Kwa ujumla, Afrika, pamoja na rasilimali zake tajiri, masoko yanayoibukia, na mahitaji makubwa ya miundombinu, inatoa fursa kubwa kwa Iran kuendeleza uhusiano wa kiuchumi. Bara hilo linaweza kuwa mshirika wa kimkakati wa Iran katika kukabiliana na vikwazo vya kimataifa. Fursa za Iran katika suala hili zinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:
Maliasili nyingi na ambazo hazijaguswa
Afrika ina 30% ya akiba ya madini ya dunia, 65% ya almasi na 60% ya dhahabu ya dunia. Rasilimali hizi kubwa, pamoja na ukosefu wa miundombinu ya kiviwanda na kiteknolojia, sambamba na uhaba wa miundomsingi ya viwanda na teknolojia ni mazingira mwafaka kwa uwekezaji na usafirishaji wa huduma za kiufundi na uhandisi za Iran. Kwa uzoefu wake katika sekta ya madini, mafuta na gesi, Iran inaweza kuchukua nafasi katika utoaji wa rasilimali hizi.

Soko linalochipukia na mahitaji bidhaa za Iran
Nchi nyingi za Kiafrika zinaendelea na zinahitaji sana bidhaa za matumizi, dawa, vifaa vya matibabu, vifaa vya ujenzi na huduma za kiufundi. Kwa uwezo wake wa uzalishaji wa ndani katika maeneo haya, Iran inaweza kuunda masoko mapya kwa mauzo yake ya nje. Pia, mauzo ya Iran ya bidhaa za kilimo, chakula na viwanda barani Afrika yana faida nono kutokana na ushindani wa bei.
Kukabiliana na vikwazo na anuwai ya mahusiano ya kigeni
Vikwazo vya kiuchumi vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran vimeweka vizingiti katika biashara na nchi za Ulaya na Marekani. Katika hali hii, Afrika, kama mshirika mpya na huru wa kiuchumi, inaweza kusaidia Iran kupunguza utegemezi wake katika masoko ya jadi. Nchi nyingi za Kiafrika pia zina uzoefu na vikwazo na ziko tayari kushirikiana na nchi zisizo za Magharibi.
Fursa za ubia na uhamishaji wa teknolojia
Kwa kuzingatia miundombinu duni barani Afrika, kuna wigo wa uwekezaji wa pamoja katika usafirishaji, nishati, kilimo na elimu. Iran kwa kupelekea teknolojia na kutekeleza miradi ya pamoja itaweza kuingiza pato na wakati huo huo kupanua ushawishi wake wa kiuchumi.
Natija
Afrika, pamoja na rasilimali zake tajiri, masoko yenye kiu, na mahitaji ya miundombinu, ni bahari ya fursa kwa Iran. Kwa mipango makini, diplomasia amilifu, na uungwaji mkono kwa sekta binafsi, Iran inaweza kuunganisha nafasi yake ya kiuchumi katika bara hilo na kutumia uwezo wake kwa ustawi endelevu.