Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: Ni lazima tufanye juhudi za kuzuia njama zozote zinazofanywa na watu baki wenye nia mbaya ya kuyaletea madhara mataifa ya Iran na Iraq.

Ali Larijan, amesema hayo mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na Qasim Al-Araji, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq aliyetembelea Iran.

Kwa mujibu wa IRIB, Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameongeza kuwa, serikali ya Iraq ni rafiki na ndugu wa karibu wa Iran. Ameongeza kwa kusema: Leo tumejadiliana masuala muhimu ya kiusalama na kuyapitia masuala tuliyoyazungumza kwa mara ya kwanza katika safari yangu ya hivi karibuni huko Baghdad, lakini masuala makuu tuliyoyazungumzia leo ni kuendelezwa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili za Iran na Iraq. Ikiwa tunataka uhusiano wa kiuchumi ubaki thabiti, lazima pia tuimarishe na kutanua uhusiano wetu katika masuala ya usalama.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran aidha amesisitizia nafasi muhimu ya Iraq katika masuala ya eneo hili la Asia Magharibi na kusema: Ni lazima tufanye jitihada za kuhakikisha tunazuia na kufelisha njama zote zinazofanywa na watu ajinabi ambao wana nia mbaya ya kuziletea madhara Iran na Iraq.

Amesema: Marekani haitaki nchi ya Iraq iwe huru. Haitaki kuiona Iraq inakuwa nchi inayojitegemea na inataka iwe chini ya udhibiti wake kwa miaka mingi. 

Kwa upande wake, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq Qasim al-Araji amejibu swali kuhusu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kwa kutumia anga ya Iraq na kusema: “Tuliushitaki utawala wa Kizayuni kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na Waziri Mkuu wa nchi yetu alisisitiza katika kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kwenye kikao na maafisa wa nchi nyingine kwamba hakuna mtu aliye na haki ya kutumia anga ya Iraq kuishambulia Iran.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *