Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeamuru viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiwamo Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika watangazwe gazetini kama njia mbadala ya wito wa kufika mahakamani kusikiliza shauri dhidi yao la kuidharau mahakama.

Wakati amri hiyo ikitolewa na Jaji Awamu Mbagwa kutokana na ombi la mawakili wa waombaji katika shauri la madai mchanganyiko namba 25480 la mwaka 2025, Heche amekamatwa na Polisi nje ya mahakama hiyo akiingia mahakamani, kwa sababu ambazo hazikuelezwa mara moja.

Shauri hilo la madai linatokana na kesi ya kikatiba inayokikabili chama hicho kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za Chadema kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema (Zanzibar) na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na katibu mkuu wa chama hicho.

Mbali ya kesi hiyo, walalamikaji wamefungua shauri la madai dhidi ya Heche, Mnyika na wenzao wakiwataka wajieleze ni kwa nini wasifungwe kama wafungwa wa madai kwa kudharau amri ya mahakama.

‎Wajibu maombi wengine ni Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya, Gervas Lyenda na Bodi ya Wadhamini wa Chadema.

Wanadaiwa kuidharau mahakama kwa madai ya kukiuka amri ya zuio iliyotolewa Juni 10, 2025 dhidi yao, inayowazuia kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali cha chama mpaka kesiya msingi itakapoamriwa.

Leo wajibu maombi watano hawakuwapo mahakamani, isipokuwa Mnyika na Azaveli Lwaitama, aliyewakilisha Bodi ya Wadhamimi wa Chadema, ambao waliwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu.

Wakili wa waombaji, Shabani Marijani anayeshirikiana na Gido Simfukwe, Mulamuzi Byabusha na Alvan Fidelis, ameieleza mahakama kuwa juhudi za za kuwafikishia wito wa mahakama kwa njia ya kawaida, wajibu maombi ambao hawakuwapo zimeshindikana. 

Amedai ni kama wanakwepa kupokea wito huo, ili kuchelewesha mwenendo wa shauri hilo.

Kwa mujibu wa kiapo cha msambaza nyaraka za mahakama, amedai alikuwa na namba zao, hivyo alipowapigia baada ya kijitambulisha walikata simu na kwa wengine alifika kwenye makazi yao, lakini hakufanikisha kuwakabidhi wito huo.

Marijani ameiomba mahakama iamuru wafikishiwe wito huo kwa njia mbadala ya kutangazwa gazetini.

Vilevile, amesema wajibu maombi wamewapatia wadai taarifa ya pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo.

Wakili Mpoki amepinga ombi la kutumia njia mbadala kufikisha wito wa mahakama, akidai kabla ya waombaji kuliwasilisha, kuna njia nyingine walipaswa kuzitumia.

Jaji Mbagwa akitoa uamuzi amekubali ombi la waombaji akaamuru watangazwe gazetini.

Amesema ingawa Wakili Mpoki amepinga kuwa waombaji bado wana njia nyingine, hakuieleza mahakama ni njia gani wanapaswa wazitumie.

“Tangazo gazetini ni njia inayotumika sana na iko ndani ya sheria kwenye amri ya V kanuni ya 16 ya Kanuni za Mashauri ya Madai,” amesema.

Jaji Mbagwa amesema mahakama imepewa nguvu ya kisheria wadaawa kupewa taarifa kwa tangazo inaporidhika kuwa hawapatikani au wanachelewesha mchakato wa mwenendo wa shauri.

“Kwa kuzingatia shauri hili limefunguliwa kwa hati ya dharura na service (upelekaji wito) ya wadaawa kwa tangazo ambalo linasomwa na kila mtu, itakuwa njia bora,” amesema na kuongeza:

“Kwa sababu hiyo naruhusu waombaji wawape wajibu maombi wito kwa njia ya tangazo kwenye gazeti linalofika sehemu kubwa ya nchi.”

Amesema shauri litaendelea Ijumaa Oktoba 24, 2025, akielekeza wadawaa wajiandae kwa usikilizwaji wa pingamizi na maombi ya msingi.

Katika pingamizi wajibu maombi wanadai kuna mgongano wa masilahi wa wakili wa waombaji wakidai ndiye aliyeshughulikia upatikanaji wa ushahidi wa kielektroniki unaodaiwa wa wajibu maombi, wakikiuka amri ya mahakama.

Pia wanadai shauri hilo limefunguliwa nje ya ukomo wa muda wa kisheria wa siku 60, vilevile wanadai amri ya mahakama inayodaiwa kukiukwa inawahusu wadaiwa kwenye kesi ya msingi pekee.

Heche akamatwa

Katika hatua nyingine, Heche amekamatwa na askari polisi katika viwanja ya mahakama. Taarifa iliyotolewa na Chadema kwa umma imesema amesafirishwa kupelekwa Tarime, mkoani Mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *